Na Sweetbert Lukonge
MSHAMBULIAJI wa
Yanga, Shabani Kondo, alionja joto ya jiwe jana baada ya kumkunja ofisa
wa jeshi la polisi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kisha
kupelekwa kituo cha polisi.
Kondo alikumbana na mkasa huo kufuatia kutaka kupigana na askari
baada ya mchezo dhidi ya Mbeya City ambao uliishuhudia Yanga ikivunja
rekodi ya Mbeya kwa kuifunga bao 1-0.
Wakati
mpira ulipomalizika, Kondo ambaye alikuwa jukwaani akiangalia mechi
hiyo, alitaka kuingia katika vyumba vya kubadilisha nguo kwa nguvu,
ndipo alipotokea askari na kumzuia lakini katika hali isiyotarajiwa,
mshambuliaji huyo alianza ‘kutunishiana naye msuli’.
Baada ya kuona hivyo, askari huyo alimkamata Kondo, akampiga pingu
kisha akamweka chini ya ulinzi, viongozi wa Yanga wakaingilia lakini
polisi waliokuwa wamemzunguka wakakataa kumuachia.
Mshambuliaji wa Yanga, Shabani Kondo (wa kwanza kushoto) akiwa chini ya ulinzi.
Wachezaji wa Yanga walipoona mambo ni magumu kwa mwenzao,
waliwazingira polisi ambao hata hivyo hawakulegeza kamba, badala yake
wakampandisha kwenye Land Rover namba PT 2072 na kumkimbiza kituoni.
Hadi tunakwenda mitamboni, haikujulikana kama straika huyo alilala ndani au aliachiwa.
Hata hivyo mmoja wa askari polisi aliliambia gazeti hili kuwa
mchezaji huyo wamemfungulia shitaka la kufanya fujo uwanjani pamoja na
kuwatolea maneno ya kashfa askari wakati wakiwa kazini wakitekeleza
majukumu yao.


Post a Comment