Moja
ya picha mbalimbli za Tembo zilipamba ukumbi yalipofanyika majadiliano
kuhusu tembo, picha hizo na ambazo zilikuwa kivutio kwa washiriki wa
majadiliano hayo ziliandaliwa na National Geograpy.
Mkurugenzi
Mtendaji wa ABC HOME Paulette Cole akiwakaribisha wanajopo na wageni
waalikwa katika majadiliano kuhusu tembo, majadiliano hayo yalifanyika
siku ya jumanne usiku Jijini New York.
Chelsea
Clinton, Makamu Mwenyekiti wa Clinton Foundation, na ambaye aliongoza
majadiliano hayo akiwatambulisha wanajopo, kutoka kushoto ni Bw. John
Heminway, Balozi Tuvako Manongi, kati kati ni Chelsea Bint wa Rais Bill
na Hilary Clinton, kulia kwa Chelsea ni Bw. Bryan Christy na anayefuatia
ni Bw. Josh Ginsberg kutoka Wildlife Conservation Society. Heminway na
Christy ni waandishi na watunga filamu na kwa pamoja wametengeneza
filamu ijulikanayo kama "The Battle for Elephants". Filamu hiyo
itaonyeshwa February 27 kupitia Channel ya National Geograpy.
Muwakilishi
wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Manongi,
akielezea jambo wakati wa majadiliano kuhusu tembo na changamoto
zinazomkabili. Balozi Manongi alitumia fursa hiyo kuelezea juhudi
mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na vitendo vya
ujangili na udhibiti wa biashara haramu ya pembe za tembo.
Bw.
Bryan Christy naye akieleza jambo, Bw. Christy ameshiriki katika
kutengeneza filamu ya The Battle for Elephants, habari zaidi zinaonyesha
kwamba sehemu ya filamu hiyo inahusu Tanzania, na Bw. Christy
anaonekana kwenye filamu hiyo akipozi kama mnunuzi wa meno ya tembo.
Sehemu ya washiriki waliohudhuria majadiliano hayo ambapo pia walipata fursa ya kuuliza maswali kwa wanajopo.
Hapana
shaka kwamba Hatari ya kutoweka kwa tembo barani afrika, ni jambo
linalowagusa wengi, washiriki wa majadiliano hayo walitumia fursa hiyo
kujifunza siyo tu hatari ya kutoweka kwa mnyama huyo, lakini pia uzuri
na sifa zake, na namna gani wanaweza kuchangia kuhakikisha hatoweki
kabisa.
Waandishi
pia walikuwepo nao walipewa changamoto ya kuandika habari zenye
kuelimisha jamii kuhusu athari za mauaji holela ya tembo pamoja na
kuihamasisha kutambua wajibu na nafasi yao katika uhifadhi wa wanyama
walio katika hatari ya kutoweka.
Pichani ni sehemu ya washiriki wa majadiliano hayo
Na Mwandishi Maalum
Zikiwa
zimepita wiki chache tangu kufanyika kwa Mkutano uliojadili kwa kina
kuhusu ujangili dhidi ya tembo na biashara haramu ya pembe za tembo
uliofanyika Jijini London, Uingereza. Jana Jumanne, hapa Jijini New
York, Marekani, palifanyika majadiliano mengine yakihusu pia sifa na
uzuri wa mnyama tembo na hatari inayomkabili.
Majadiliano
hayo na ambayo yaliwavutia washiriki wengi, yaliandaliwa kwa
ushirikiano kati ya National Geograpy na ABC na yalifanyika katika jengo
lijulikanalo kama ABC HOME lilipo Broadway, jijini New York.
Balozi
Tuvako Manongi, Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika Umoja wa Mataifa, alikuwa kati ya wanajopo wanne
walioalikwa kushiriki majadaliano hayo ambayo yaliongozwa na Chelsea
Clinton, Makamu Mwenyekiti wa Clinton Foudantion.
Wanajopo
wengine walikuwa ni Bw. Josh Ginsberg kutoka Wildlife Conservation
Society, Bw. John Heminway mwandishi na mtengeneza filamu ambaye pamoja
na mwanajopo mwingine Bryan Christy wameshiriki katika kutengeneza
filamu ijulikanayo kama “The Battle for Elephants” filamu hii
inatarajiwa kuonyeshwa february 27 kupitia Channel ya National Geograpy.
Wanajopo
hao wakiongozwa na Chelsea Clinton, walipata fursa ya kila mmoja wao
kuelezea nini yeyé kama mtu binafsi au kupitia taasisi anayoiwakilisha
ametoa mchango gani katika suala zima la uhifadhi wa Tembo na uthibiti
wa mauaji holela ya Tembo na biashara haramu ya pembe za tembo.
Balozi
Manongi kwa upande wake, alielezea juhudi mbalimbali ambazo serikali
inafanya katika kukabiliana na ujangili dhidi ya tembo, pamoja na
biashara haramu ya pembe , aidha alielezea dhamira na nia ya serikali ya
kuendeleza mapambano ya kuwanusuru tembo kupitia awamu ya pili ya
Operesheni Tokomeza.
Balozi
pia alijibu maswali mbalimbali na kutolea ufafanuzi hoja zikiwamo
kuhusu kwanini operesheni tokomeza ilisitishwa, na je serikali ilikuwa
na mpango gani kuhusu shehena ya pembe za ndovu ambayo iko katika
maghala.
Kwa
ujumla wanajopo wote walikubaliana kwamba, mapambano dhidi ya ujangili
na biashara haramu ya pembe za ndovu ni vita ngumu hasa ikizingatiwa
kwamba mtandao unaohusika na biashara ya pembe za tembo ni mpana sana na
unaohusisha watu wengi.
Na kwa
sababu hiyo wamehimiza mambo kadhaa yakiwamo, ushiriki wa wadau kutoka
makundi mbalimbali ya kijamii kitaifa na kimataifa, udhibiti wa soko na
hitajio la pembe za ndovu, utoaji wa elimu kwa umma, uwezeshwaji wa
watendaji katika ngazi mbalimbali, na uimarishaji wa sheria.
Post a Comment