Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
akiwa kwenye picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa India Mohamed Hamid
Ansari wakati walipokuwatana nchini India.
*******
Tanzania
na India zimeeleza kuridhishwa na uhusiano na ushirikiano uliopo baina
yao na kusisitiza dhamira ya kweli ya kuona kuwa ushirikiano huo unazidi
kuimarika kwa manufaa ya Serikali na wananchi wa nchi hizo.
Hayo
yamejitokeza leo wakati wa mazungumzo kati ya Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa
Rais wa India Mohamed Hamid Ansari.
Katika
mazungumzo hayo viongozi hao wamesema kuwa uhusiano wa kidiplomasia
kati ya nchi hizo ulioanzishwa mwanzoni mwa miaka ya sitini umekuwa
ukiimarika mwaka hadi mwaka kwa kuongeza maeneo ya ushirikiano katika
nyanja mbalimbali za uchumi na kijamii.
Wameeleza
kuwa ziara za viongozi wa nchi hizo pamoja na ziara za mara kwa mara
katika ngazi ya mawaziri ni uthibitisho wa uhusiano huo mzuri kati ya
nchi hizo.
Katika
mazungumzo hayo Dk. Shein ameupongeza ushirikiano uliopo kati ya
Zanzibar na India na ameishukuru Serikali na wananchi wa India kwa
misaada mbalimbali ambayo imekuwa ikiitoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na wananchi wake.
Dk.
Shein alimueleza Makamu wa Rais wa India kuwa ziara yake nchini humu
imelenga kuimarisha uhusiano huo wa kidiplomasia uliasisiwa miaka ya
sitini chini ya misingi imara ya urafiki iliyowekwa na waasisi wake
viongozi wa kwanza wa nchi mbili hizo.
Halikadhalika
alimueleza kuwa ziara hiyo amedhamiria kukukuza ushirikiano kati ya
Zanzibar na India katika maeneo ya elimu, mafunzo, biashara, kilimo
pamoja na kuhimiza uwekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi.
Alifaanua
kuwa uhusiano na ushirikiano kati ya watu wa Zanzibar na watu wa India
ni wa kihistoria uliodumu kwa karne nyingi hivyo kuufanya kuwa wa
kidugu.
Amemueleza
Bwana Ansari kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefurahishwa na
msaada wa ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali kitakachojengwa huko Pemba
pamoja na makubaliano yaliyofikiwa jana ya kuanzisha Chuo kama hicho
huko Unguja kupitia Chuo cha Barefoot cha Tilonia, Jaipur.
Amebainisha
kuwa katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na wananchi wengi wa
Zanzibar wanakwenda India kwa sababu za kimatibabu hivyo ametaka kuwepo
na ushirikiano zaidi wa namna bora ya kuleta wagonjwa hao nchini humu.
Kwa
upande mwingine Dk. Shein ameiomba Serikali ya India kuangalia namna
inavyoweza kushirikiana na Serikali ya Zanzibar kuisaidia upatikanaji wa
madawa kwa Zanzibar.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ametumia fursa
kumueleza Makamu wa Rais wa India haja ya kuongeza fursa zaidi za masomo
ya muda mfupi na muda wa kati kwa wananchi wa Zanzibar ili kujenga
uwezo katika taaluma mbalimbali ili kuharakisha maendeleo.
Kwa
upande wake Makamu wa Rais wa India Bwana Mohamed Hamid Ansari
amemhakikishia Dk. Shein kuwa Serikali ya nchi yake itaendelea kusaidia
jitihada zinazofanywa na Serikali na wananchi wa Zanzibar za kujiletea
maendeleo.
Bwana
Ansar amesema uhusiano wa kihistoria wa wananchi wa India na Zanzibar
ulioanza karne nyingi tangu enzi za kutegemea pepo za Kusi na Kaskazi
umekuwa imara na kila siku wananchi wake wameonyesha ari ya kuzidi
kuuimarisha.
Mapema
asubuhi alitembelea makumbusho ya Mahatma Ghandi iliyopo mjini New
Delhi ambapo aliweka shada la maua pamoja na kusaini kitabu cha
kumbukumbu.
Baadae
mchana anatarajiwa kukutana na watanzania anaoishi mjini hapa katika
ukumbi wa Urafiki kwenye hoteli ya Ashok na atakutana pia na Waziri wa
Afya na Ustawi wa Familia wa India. Jioni atahudhuria chakula cha jioni
kilichoandaliwa kwa heshma yake na mwenyeji wake Makamu wa Rais wa
India.
Hapo
jana kabla ya kuondoka Jaipur, Jimbo la Rajastan, kuja New Delhi Dk.
Shein alitembelea makumbusho ya Hawa Mahal na Albert yaliyopo mjini
humo.
Miongoni
mwa waliofuatana na Rais katika ziara hiyo ni pamoja na Mke wake Mama
Mwanamwema, Waziri wa Fedha Omar Yusuf Mzee, Waziri wa Uwezeshaji,
Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Zainab Omar Mohamed,
Waziri wa Biashara na Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Marzui, Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dk. Mahadhi Juma
Maalim na Balozi wa Tanzania nchini India Injinia John Kijazi.
Wengine
ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Mohamed Saleh Jidawi, Katibu Mkuu Kilimo
na Maliasili Affan Othman Maalim, Mshauri wa Rais Ushirikiano wa
Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi Balozi Mohamed Ramia na Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar –ZIPA Salum Khamis Nassor.



Post a Comment