Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.PICHA|MAKTABA
Waraka huo wa kurasa 22 unaoainisha mambo yenye masilahi kwa chama hicho, unawataka wajumbe wake kuutetea bungeni.Gazeti
hili limefanikiwa kuona waraka huo, ambao pamoja na mambo mengine,
umetoa mapendekezo katika ibara 42 za Rasimu ya Katiba ya Tume na
kupangua hoja nyingi.
Katika
miongoni mwa hoja hizo, chama hicho kimesisitiza muundo wa Muungano wa
Serikali mbili lakini kikapendekeza kuwapo Baraza la Wawakilishi la
Tanzania Bara. Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu waraka huo, Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliukana akisema pamoja na msimamo
wa chama hicho kuwa ni Serikali mbili, hakijafikia hatua ya kuwa na
waraka.Alisema vikao vya juu vya chama
huwa havitoi waraka, bali msimamo na kwamba vyombo vingine vya chama
ndivyo hutoa waraka, lakini hadi sasa havijafikia hatua hiyo.Alisema
kuwa alipoeleza maazimio ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC),
alitaja msimamo wa chama hicho kuwa ni Serikali mbili zilizoboreshwa,
lakini hakutaja maboresho hayo hata pale alipoulizwa na waandishi wa
habari kwa sababu hayakuwa yamekamilika.Hata
hivyo, wajumbe watatu wa NEC kwa nyakati tofauti waliomba wasitajwe
gazetini walisema mambo yaliyomo kwenye waraka huo ndiyo waliyokubaliana
lakini hakuwa na uhakika kama ulishasambazwa.
Kwa
mujibu wa waraka huo, chama hicho kinadaiwa kuainisha mambo
kiliyopendekeza katika Rasimu ya Kwanza na jinsi yalivyoshughulikiwa
katika Rasimu ya Pili ya Katiba.
Pia, kimeeleza mambo mengine mapya na kubainisha kasoro zake, ikiwamo utata katika mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi.
Waraka
huo pia unazungumzia sura mpya ya 17 katika Rasimu ya Katiba, ukisema
inazungumzia mambo ya mpito kuelekea kupata Katiba Mpya, lakini gharama
za utekelezaji wake hazitabiriki.
Sababu za Serikali mbili
Katika
waraka huo, CCM kinadaiwa kueleza kuwa mapendekezo yake kuhusu muundo wa
serikali mbili hayatokani na sera yake pekee, bali pia udhaifu
uliojionyesha katika pendekezo la muundo wa Serikali tatu.
“Hivyo
basi, CCM inapendekeza kwamba mfumo wa serikali mbili ufanyiwe
marekebisho ambayo yatashughulikia changamoto zilizopo,” imesema sehemu
ya waraka huo.
Wakati
CCM kikitaka Muungano wa serikali mbili, Rasimu ya Pili ya Tume
inapendekeza serikali tatu, sawa na zile zinazopigiwa chapuo na vyama
vya Chadema na CUF.
Idadi ya
Serikali katika muundo mpya wa Muungano, bado ni changamoto kutokana na
hatua ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kugawanyika katika makundi
yenye mitazamo tofauti.
Makamu wa Rais
Katika
mfumo huo wa serikali mbili, waraka huo umependekeza Rais wa Zanzibar
kuwa Makamu wa Rais bila kujali kama Rais wa Jamhuri ya Muungano anatoka
Bara au visiwani humo.
“Rais wa
Zanzibar katika Muungano, awe Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
ambaye atakuwa na msaidizi wake kwa masuala ya Zanzibar na mmoja wa
viongozi wakuu wa nchi,” imesema sehemu ya waraka huo na kuongeza:
“Hii
itaongeza na kuweka wazi madaraka ya Rais wa Zanzibar ndani ya Serikali
ya Muungano na nje ya nchi,” imesema sehemu ya waraka huo.
Muundo wa Bunge
Kuhusu
Bunge, waraka huo unapendekeza kuwe na Baraza la Wawakilishi la Tanzania
Bara kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Bara tu.
“Katika
pendekezo hili, majimbo ya Jamhuri ya Muungano yaundwe upya na majimbo
ya uchaguzi ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar yawe ndiyo hayohayo
majimbo ya uchaguzi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano,” ulisema waraka
huo.
Waraka
huo umependekeza Bunge la Muungano wakati linajadili mambo ya Muungano,
wabunge wote washiriki majadiliano na inapofika kujadili mambo ya
Tanzania Bara, washiriki wabunge wanaotoka Bara tu.
“Kama
Spika anatoka sehemu moja ya Muungano, Naibu wake atatoka upande wa pili
na wakati wa vikao vya masuala ya Bara Spika/Naibu Spika anayetoka Bara
ndiye atakayeendesha kikao,” sehemu ya waraka huo inasema.
Waraka huo umependekeza masuala yasiyokuwa ya Muungano, kushughulikiwa na wabunge wa Tanzania Bara pekee.
Muundo wa mawaziri
Waraka
huo umependekeza wajumbe wa Bunge la Muungano kuwa mawaziri wa wizara za
mambo ya Muungano tu na wizara zisizo za Muungano ziongozwe na wabunge
wanaotoka Tanzania Bara tu.
Pia
umependekeza orodha ya mambo ya Muungano ambayo yatakuwa katika Katiba
na mambo yasiyokuwa ya Muungano yaorodheshwe katika sheria
itakayoainisha pia usimamizi, utekelezaji na gharama zake.
Mahakama
Kwa upande wa muundo wa Mahakama ya Juu, waraka umependekeza ndani ya mahakama hiyo kuwe na kitengo cha masuala ya Katiba tu.
Kuhusu
misaada na mikopo nafuu kutoka kwa wahisani, umependekeza Serikali ya
Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar, zijadili kwa kina kanuni ya
mgawanyo wa fedha zinazotokana na vyanzo hivyo.
“Kuwekwe
utaratibu wa kisheria wa kutenganisha misaada inayoelekezwa kwenye
miradi ya Muungano na isiyokuwa ya Muungano,” ilisema sehemu ya waraka
huo.
Usimamizi wa Muungano
Waraka
huo umependekeza kuwapo kwa Tume ya Usimamizi na Uratibu wa mambo ya
Muungano kikatiba na uendeshaji wake, kadhalika na mwenendo wa sasa wa
vikao vya pamoja vinavyohusu kero za Muungano.
“Uratibu
na usimamizi wa masuala ya Muungano uwekwe kisheria na Tume ipewe
mamlaka ya kuzisimamia taasisi zote za Muungano katika makubaliano
yatakayofikiwa na pande zote mbili,” unasema waraka huo.
Kuhusu
Tume ya Pamoja ya Fedha, waraka huo unasema tume hiyo ambayo imetamkwa
katika Katiba na kupitishwa na Sheria ya Bunge, imeshaundwa na mamlaka
yake yanafahamika.
“Tunapendekeza
Tume hii ipewe nguvu zaidi, iwekewe mfumo madhubuti wa kuiendesha na
kuisimamia kwa karibu. Mapendekezo yanayotolewa na Tume yashughulikiwe
na serikali zote mbili kwa haraka ili kama hakuna kikwazo, mapendekezo
yake yatekelezwe bila kuchukua muda mrefu,” unasema.
Pia
waraka huo umependekeza kufunguliwa kwa akaunti ya pamoja ya fedha
zitokanazo na mapato ya vyanzo vya Muungano, kama ilivyoainishwa katika
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwapo kwa utaratibu wa
kisheria utakaoelekeza uendeshaji wa akaunti hiyo na kuweka mgawanyo wa
mapato hayo kwa pande mbili za Muungano.
“Hii
itasaidia sana kuwianisha uchumi wa pande hizo mbili. Sheria kuhusu
utaratibu huo isimamiwe na Tume ya Uhusiano na Uratibu kama
ilivyopendekezwa katika rasimu,” waraka huo unasema.
MWANANCHI
Post a Comment