Katibu
Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini, Joyce Fisoo akizungumza na wadau wa
filamu nchini (hawapo pichani) wakati akipitia na kukagua filamu ya Dark
Forest ya Kikundi cha Harakati kwenye ofisi za Bodi hiyo jijini Dar es
Salaam leo.
Katibu
Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini, Joyce Fisoo akiwaeleza jambo
Mkurugenzi wa Kikundi cha Harakati Fatia Musa (katikati) na Mjumbe wa
kikundi hicho na Mwigizaji wa filamu hiyo Ramadhani Nassoro kuhusu
filamu yao inayoitwa Dark Forest, kwenye ofisi ya Bodi hiyo jijini Dar
es Salaam leo.Mkurugenzi
wa Kikundi cha Harakati Fatia Musa, akitia saini makubaliano ya
kutekeleza maazimio waliokubaliana na Bodi kuhusu kurekebisha filamu
hiyo huku akishuhudiwa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini Joyce
Fisoo.
Mwigizaji
wa filamu hiyo Ramadhani Nassoro, akitia saini makubaliano ya
kutekeleza maazimio waliokubaliana na Bodi kuhusu kurekebisha filamu
hiyo huku akishuhudiwa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini.
Picha zote na Hussein Makame-MAELEZO.
……………………………………………………………………………………………….
Hussein Makame-MAELEZO
BODI
ya Filamu imewaonya wazalishaji wa filamu nchini kuwa watakaotengeneza
filamu chini ya kiwango kwa makusudi watafungiwa ikiwa ni moja ya njia
ya kuboresha tasnia ya filamu nchini na kukuza vipaji vya wasanii
wachanga.
Onyo
hilo limetolewa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini, Joyce
Fissoo baada ya kupitia na kuikagua filamu ya Dark Forest ya Kikundi cha
Harakati ambayo imeonekana imetengenezwa chini ya viwango
vinavyotakiwa.
Alisema
utengenezaji wa filamu hiyo haikutumia vifaa vya kitaalamu, ina mwanga
mbaya, haikutumia vifaa vya sauti vya kitaalamu na kufanya kuingiliana
kwa sauti nyingine zisizohitajika na kasoro nyingine nyingi.
Fissoo
alisema Bodi hiyo pia ilibaini kuwa uchukuaji wa picha wa filamu hiyo
ulitumia siku tatu jambo ambalo ni kuidhalilisha tasnia ya filamu na
kutowatendea haki Watanzania ambao ndio watumiaji wa kazi hiyo.
“Baada
ya kupitiwa ilibainika filamu hiyo kuwa katika kiwango cha chini sana
na kwamba Kampuni ya Lee One Production ilishiriki kuchukua picha zake
ni kampuni yenye uzoefu na kazi zake zilikwishawahi kuja Bodi zikiwa
katika kiwango cha kuridhisha” alisema Fissoo.
Akizungumza
kwa njia ya simu na MAELEZO, Mkurugenzi wa Lee One Production Emmanuel
Mapunda alisema awali filamu hiyo ilirekodiwa vizuri lakini kanda ya
picha za filamu hiyo haikutunzwa kwenye vifaa bora kama alivyoshauri.
Alisema
baada ya kugundua kuwa picha za filamu hiyo zimeharibika, aliwashauri
wahusika wa filamu hiyo kutoitoa kutokana na kutokuwa na viwango
vinavyohitajika na kwamba wanatakiwa wakairekodi upya, hata hiyo
hawakukubaliana.
Kutokana
na filamu hiyo kutengenezwa chini ya kiwango, Fissoo aliitisha kikao
kukutana na kikundi cha Harakati kilichotoa filamu hiyo na wahusika wote
kujadiliana nao kwa kina, walifikia maazimio kuwa tabia ya kuharibu kwa
makusudi kazi za wasanii wanaoibukia iachwe mara moja.
“Wanaotengeneza
filamu chini ya kiwango kwa makusudi watafungiwa, onyo kali kwa
Mkurugenzi wa kampuni ya Lee One Production na Mwongozaji wa filamu
husika Bwana Ramadhani Kishoka kwa kutotekeleza majukumu yao kwa
kuzingatia weledi na taalum” alisema Fissoo na kuongeza :
”Marekebisho
hayo yafanyike kwa kuzingatia viwango vya ubora kwani kuipeleka sokoni
filamu hiyo ni kutowatendea haki Watanzania na kuiua tasnia ya filamu
jambo ambalo Serikali haitaliruhusu”.
Waandaaji
wa filamu hiyo walikiri kuwa kiwango cha filamu hiyo ni cha chini na
muongozaji wake Ramadhani Kisoka ameahidi kuwa ataandika barua ya kuomba
radhi na kurudia kazi hiyo na kuiwasilisha Bodi.
Bodi
ya Filamu imekuwa ikitekeleza majukumu yake ikiwemo kupitia na kukagua
filamu zinazotengenezwa nchini na kuzipitisha kwenda sokoni ambapo
filamu hiyo ya Dark Forest ilikamatwa na Bodi wakati wa operesheni zake
za kawaida
Post a Comment