***********
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ameikosoa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, akidai imeshindwa kuwasilisha kwa usahihi maoni
yaliyotolewa na wananchi.
Alisema Tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Jaji
Joseph Warioba iliwasilisha maoni yaliyokuwa yakiunga mkono mlengo wake
badala ya maoni halisi yaliyotolewa na Mabaraza ya Katiba.
Madai hayo mapya ya Kinana yamekuja wakati tayari Tume hiyo imevunjwa rasmi na Rais, kwa mujibu wa sheria.
“Kulikuwa na utaratibu wa kupata maoni kutoka
kwenye mabaraza na kuna kata zilihojiwa, tume haijatuambia kwa sababu
gani hawakuyasema wanayoyataka wao,” alisema Kinana.
Alisena kuwa kulikuwa na mabaraza 171, lakini Tume
pia ilishindwa kutoa takwimu za watu wangapi walikuwa wakiunga muundo
wa muungano wa serikali mbili au tatu katika mabaraza hayo.
“Majaji walisema masilahi ya nchi yapo kwenye
serikali mbili na wakuu wa mikoa hali kadhalika, lakini mbona Tume
hawakusema hayo?” alihoji Kinana.
Katibu Mkuu huyo alikuwa akizungumza katika
mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CCM Mkoa wa Dar es Salaam jana,
kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa hotuba aliyoitoa katika Bunge Maalumu
la Katiba hivi karibuni.
Alisema chama chake kinaunga mkono mchakato wa kupata Katiba Mpya, lakini lazima wahakikishe katiba hiyo ni ya wananchi.
Hii ni mara ya pili kwa viongozi wa juu wa chama
hicho kukosoa takwimu za Tume, mara ya kwanza Rais Kikwete alitilia
shaka takwimu zilizomo katika ripoti ya Tume hiyo wakati akitoa hotuba
yake bungeni.
Kinana alisema pamoja na kuhoji weledi wa Tume ya
Warioba pia alitetea hoja ya wingi wa wajumbe wa CCM katika Bunge
Maalumu la Katiba.
“Kuna watu kila siku wanalia eti wao wapo wachache
na sisi tupo wengi, hii ni lugha ya ajabu kweli kweli, usiku na mchana
wanakutana kujadiliana na walipoona chama kimoja kimoja hakiwezi
wakaanzisha Ukawa.
“Hao wanaosema tunatumia wingi kupinga masilahi ya
nchi, sasa ni masilahi gani yasiyowahusisha CCM?” alihoji Kinana huku
akishangaliwa na wafuasi wa chama hicho.
MWANANCI
Post a Comment