WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda ameitaka Wizara ya Maji itafute njia mbadala
zitazosaidia kupunguza gharama za kuchimba visima ili wananchi waweze
kupata maji safi na salama.
“Wizara
ya Maji angalieni uwezekano wa kupunguza gharama za uchimbaji wa visima
ili wananchi waweze kumudu kuchimba visima na wapate uhakika wa maji
safi na salama,” alisema.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Machi 23, 2014), wakati akifunga
Maadhimisho ya Wiki ya Maji Kitaifa yaliyofanyika kwenye Uwanja wa
Jamhuri mkoani Dodoma.
“Hivi
sasa nimeambiwa gharama ya kuchimba kisima mita moja ni sh. 150,000/.
Je kama mtu anataka kuchimba kisima chenye urefu wa mita 180 au 200
itakuwaje? Ni dhahiri kuwa watu hawataweza kumudu hizo gharama.
Angalieni namna ya kuzipunguza,” alisisitiza.
Waziri
Mkuu ambaye alikuwa akifunga maadhimisho hayo kwa niaba ya Rais Jakaya
Kikwete aliwataka wakazi wa mkoa wa Dodoma waendelee kuthamini dhana ya
uchangiaji ili waweze kumudu kuendeleza miradi hiyo.
Aliwataka
pia watunze vyanzo vya maji na kutunza miundombinu pamoja na mitambo
iliyonunuliwa kuendesha visima mbalimbali kwani maji yana gharama.
“Ninawasihi sana muitunze mitambo iliyowekwa kuendeshea visima hivi
kwani ni vifaa vya gharama sana,” aliongeza.
Mapema,
Waziri Mkuu alizindua kisima cha maji kwenye kijiji cha Mkonze nje
kidogo ya mji wa Dodoma ambacho ujenzi wake umegharimu sh. milioni
519.6/-. Kisima hicho chenye vichoteo 15, kitawanufaisha wakazi 5,887
kati ya 6,869 sawa na asilimia 85.7 ya wakazi wa kijiji hicho.
“Kabla
ya kujengwa kisima hiki, ndoo ya maji ya lita 20 ilikuwa ikiuzwa sh.
500/- lakini sasa ndoo moja inauzwa kwa sh. 100/- tu,” alisema Mhandisi
Mohammed Kali wakati akitoa taarifa ya mradi huo kwa Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu pia aliweka jiwe la msingi kwenye tenki la maji katika Chuo Kikuu
cha Dodoma (UDOM) lenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 4,500. Ujenzi
wake unatarajiwa kukamilika Novemba, 2014.
Akizungumza
na wanajumuiya ya UDOM walioshiriki uzinduzi huo, Waziri Mkuu alisema
mradi huo mkubwa unaenda sambamba na ujenzi wa mradi mwingine mkubwa wa
maji taka (recycling plant). “Ninawasihi muangalie uwezekano wa kutumia
maji machafu yatakayosafishwa ili yatumike kumwagilia miti na maua
muweze kutunza mandhari ya UDOM,” alisema.
Akizungumza
katika hafla ya uzinduzi wa tenki hilo, Waziri wa Maji, Prof. Jumanne
Maghembe alisema hadi kukamilika kwake, mradi huo utagharimu sh. bilioni
28. Alisema mradi huo unaojumuisha ujenzi wa miundombinu ya maji safi
na maji taka katika Chuo hicho, umefanyika chini ya Mpango wa Kuendeleza
Sekta ya Maji nchini (WSDP).
Naye
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Tanzania,
Burundi na Uganda, Bw. Phillippe Dongier alisema wao kama wadau wa
maendeleo, wanaona fahari kushirikiana na Wizara ya Maji katika kuleta
maendeleo ya sekta hiyo kwa Watanzania.
Uzinduzi
wa miradi hiyo ya maji ni sehemu ya miradi 13 iliyopangwa kuzinduliwa
mkoani Dodoma kwenye maadhimisho ya maji ya mwaka huu. Hata hivyo, mkoa
huo una miradi 69 ya maji ambayo ujenzi wake unaendelea kwa awamu
tofauti.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAPILI, MACHI 23, 2014
Post a Comment