WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano), Bw. Stephen Wassira aliwavunja mbavu
waombolezaji waliofika kwenye mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara
marehemu John Gabriel Tuppa yaliyofanyika nyumbani kwake Kilosa mjini,
mkoani Morogoro.
Akitoa
salamu za rambirambi kwa niaba ya wabunge wa mkoa wa Mara, Bw. Wassira
alisema watu wote waliohudhuria mazishi hayo wanataka kwenda peponi
lakini tatizo ni masharti yanayoambatana na hiyo safari.
“Baba
Askofu Mkude (Telesphor), ukiuliza nani anataka kwenda peponi, wote
hapa watanyoosha mikono, lakini tatizo ni masharti yanayoambatana na
safari ya kwenda huko peponi. Kila mtu anaona ugumu wa hayo masharti
ukiwemo wewe Baba Askofu,” alisema huku umati uliokuwepo ukiangua
vicheko.
Alisema
kifo hakizoeleki wala hakizuiliki na kwamba hakuna anayeweza
kuchakachua siri ya Mwenyezi Mungu kuhusu uhai wa maisha ya wanadamu.
Aliwaombea wafiwa wapate faraja katika kipindi hiki kigumu.
Akizungumza
na waombolezaji wakati wa ibada ya mazishi nyumbani kwa marehemu, jana
jioni(Jumamosi, Machi 30, 2014), Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema
amemfahamu marehamu Tuppa tangu mwaka 1993 alipoteuliwa kuwa Mkuu wa
Wilaya kwa mara ya kwanza.
“Marehemu
Tuppa amekuwa mtumishi Serikalini kwa muda wa miaka 42 na katika muda
wote huo, miaka 21 ya utumishi wake ameitumia akihudumia wananchi kama
Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa. Alikuwa ni mtu mwema, aliyejali watu na
wala hakuwa na tamaa za hovyo hovyo,” alisema Waziri Mkuu.
“Kumpoteza
mume na baba ni mtihani mkubwa lakini mkimtumaini Mwenyezi Mungu
mtafaulu,” alisema Waziri Mkuu na kuwasihi mjane wa marehemu Tuppa
pamoja na watoto wasisononeke wanapopatwa na jambo na wala wasisite
kumuona Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, yeye binafsi ama Rais Jakaya Kikwete
kwa msaada zaidi.
Mapema,
akiongoza ibada hiyo ya mazishi, Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro,
Mhashamu Telesphor Mkude aliwataka watu waliohudhuria mazishi hayo
kufanya toba kama njia ya kuleta mabadiliko kwenye maisha yao.
“Ninawaomba
kila mmoja mahali hapa afanye toba, awe mkweli, asifanye uchakachuaji…
kila mtu kwa imani yake aacha mabaya na atende mema kama ndugu yetu John
Tuppa ambaye alijitoa na kufanya zaidi kwa ajili ya wengine,” alisema.
Aliwataka
watu wote wajihoji njia zao kama ni kamilifu, na kwamba ni kwa vipi
wanawatendea watu wengine wanaohusiana nao iwe ni baba, mama, watoto au
hata maofisini na kwenye biashara.
“Je
mnawaongozaje watu katika ofisi zenu katika ngazi mbalimbali, iwe ni
wizarani, mkoani, wilayani hadi kwa mtendaji wa kijiji? Je unawafanyaje
watu katika biashara unayofanya? Je unawadhalilisha kwa kuwauzia vitu
vibovu? Je unawauzia madawa ya kulevya?” alihoji Askofu Mkude.
Aliwataka
watu wote kila mmoja kwa imani yake waendelee kuuombea mchakato wa
Katiba ili iweze kupatikana Katiba bora zaidi. “Tuna wajibu kama wacha
Mungu tuwaombee wajumbe wa Bunge maalum ili kazi ile ifanyike sawa na
mapenzi ya Mungu. Tusipowaombea watafanya vitu vya ajabu,” alisisitiza.
Mazishi
hayo yalihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal,
baadhi ya mawaziri, wabunge wa mikoa ya Mara na Morogoro, wakuu wa mikoa
mbalimbali, viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya siasa.
Bw.
Tuppa alizaliwa Januari mosi, 1950. Amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya za
Chunya, Mwanga, Bukoba, Muleba na Dodoma kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa
Mkoa wa Mara mwaka 2011. Ameacha mjane, watoto watano na wajukuu
watano.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAPILI, MACHI 30, 2014
Post a Comment