Nabii Josephat Mwingira. |
Rais Jakaya Kikwete ameagiza kurejeshwa
kwa shamba la ekari takribani 12,000 kwa wananchi ambalo liliuzwa kwa
taasisi ya Efatha Ministry inayoongozwa na Nabii Josephat Mwingira.
Agizo hilo la Rais Kikwete limetolewa
jana kupitia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman
Kinana wakati akiwahutubia wakazi wa Kata ya Moro katika Kijiji cha
Mawenzusi.
Wakati akiwasili kijijini hapo Kinana
alipokewa na mabango yenye ujumbe unaozungumzia kilio cha wananchi
kudhulumiwa shamba hilo.
Wananchi hao wakiongozwa na Mbunge wao wa
Sumbawanga Mjini, Hillary Aeshi pamoja na Diwani wa Kata hiyo ya Moro,
Festo Mwananjela, waliwasilisha kilio chao kuhusu unyang'anyi wa shamba
hilo na taasisi hiyo ya Efatha, hali ambayo imewaacha wakazi wa eneo
hilo bila kuwa na eneo lolote la kufanyia shughuli za kilimo.
Akizungumza katika mkutano huo wa
hadhara, Mwananjela alisema shamba hilo kabla ya kutaifishwa na Serikali
lilikuwa ni maeneo ya kilimo ya wakazi wa eneo hilo, lakini baadae
lilichukuliwa na Serikali kwa ajili ya kuendelezwa, hata hivyo Serikali
ilishindwa kuliendeleza na kuliuza kwa taasisi hiyo.
"Cha kushangaza ni muda mrefu tangu
shamba hilo kuuzwa kwa taasisi hiyo, lakini hakuna shughuli zozote
zinazoendelea kwenye mashamba hayo huku wananchi wa maeneo hayo
wakinyanyaswa na kupigwa pindi wanapotumia njia zilizomo ndani ya shamba
hilo ambazo walikuwa wakitumia tangu awali," alisema.
Naye Mbunge Aeshi alimuonesha Kinana,
kijana Nuru Togwa aliyekatwa masikio yote mawili na walinzi waliowekwa
kwenye shamba hilo wakati akipita akitoka kijijini kwake kuelekea
Sumbawanga Mjini.
Kinana akizungumzia sakata hilo alisema,
wananchi hao kutokurejeshewa shamba hilo na Serikali ni dhuluma na
haikupaswa kuliuza shamba hilo bila kushirikisha wananchi hao.
"Serikali ilitakiwa iombe radhi wananchi
baada ya kuona imeshindwa kuliendesha shamba hili, ingelirejesha kwao na
si kuliuza kwa mwekezaji mmoja na kuacha watu 16,000 wakiwa hawana
sehemu yoyote ya kufanyia shughuli zao kilimo, hii si haki," alisema.
Aidha, alionya juu ya watu wanaojiita
wawekezaji ambao wanakuja nchini na kuchukua maeneo makubwa ya ardhi ya
wananchi kwa madai ya kuwekeza na badala yake wamekuwa wakitumia
mashamba hayo kukopea na kujinufaisha wenyewe na si kufanya shughuli
iliyokusudiwa.
Alisema kuna watu wengi wanaojiita
wawekezaji wako maeneo mengi na si mkoani Rukwa peke yake, ambao
wamejichukulia maeneo hayo kwa kigezo cha jina la uwekezaji na matokeo
yake nchi imekuwa na maeneo makubwa yasiyoendelezwa huku wananchi wa
maeneo husika wakitaabika kwa kukosa ardhi.
"Serikali inayaona haya lakini imekaa
kimya, hii ni dhambi inayohitaji kusahihishwa haiwezekani sehemu kubwa
ya mashamba asilimia 70 nchini yaliyokabidhiwa kwa wawekezaji iwe
haifanyiwi lolote, kwani kama wangefanya inavyokusudiwa kwa kuendeleza
shughuli za kilimo Tanzania isingekuwa na njaa," alisema.
Kinana aliwahakikishia wakazi hao kwamba
Tume ya Mkoa iliyoundwa kwa ajili ya kufuatilia suala hilo mapendekezo
yake ambayo ni kutaka kurejeshwa kwa shamba hilo mikononi mwa wananchi
na mwekezaji huyo kupatiwa sehemu kidogo yanafanyiwa kazi.
Kabla ya kuondoka mkutanoni hapo Kinana
aliwatangazia wakazi hao kwamba tayari amezungumza na Rais Kikwete
ambaye ameridhia shamba hilo lirejeshwa mikononi mwa wananchi ili
waendelee na shughuli zao za kilimo.
Post a Comment