Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Utata bungeni

 

    Yazuka madai ya kughushi saini za Nyerere
  • Yazuka madai ya kughushi saini za Nyerere, Msekwa

WAKATI Kamati za Bunge Maalumu la Katiba zikianza rasmi kujadili rasimu ya katiba, hati za Muungano zimeibua utata ambapo saini za Rais wa Kwanza, hayati Julius Nyerere na aliyekuwa Katibu wa Bunge, Pius Msekwa zinatofautiana na saini zao halisi.
Baadhi ya kamati za Bunge zina nakala wakati nyingine zimenyimwa nyaraka hizo, huku baadhi ya wajumbe wakipinga sheria za hati za Muungano kwa madai kuwa saini za Nyerere na Msekwa zimeghushiwa.
Wanasema zimechongwa kwa utaalamu wa kompyuta.
Mathalani katika hati ya Tanganyika No.22 ya 1964, herufi mbili za jina la Julius (us) zinatofautiana na herufi nne za mwanzo (Juli) wakati kwenye hati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania No.18 ya 1965 herufi zote zimeandikwa kwa ufanano.

Utata mwingine upo kwenye herufi K ya jina la katikati la Kambarage. Katika hati ya mwaka 1964 herufi hiyo inatofautiana na ile ya mwaka 1965.
Hata saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri wakati huo, Pius Msekwa inatofautiana kwenye hati hizo, na hivyo wajumbe kadhaa wametaka ziletwe hati halisi badala ya nyaraka za sheria zilizoidhinisha Muungano.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wenyeviti wa kamati hizo, Ummy Mwalimu (1), Anne Kilango, Malecela (11), na Kidawa Hamis Salehe (9) walikiri utata huo wa hati za Muungano.
Mwalimu alisema kwenye kamati yake wajumbe waliomba kupatiwa nyaraka hizo na baada ya muda mfupi zilipatikana.
Kilango alisema ziligawiwa lakini wajumbe wakabishana kuhusu utata wa saini.
“Nashukuru kulikuwa na mwanasheria wa Zanzibar ambaye ni mjumbe wa kamati yangu. Aliziangalia nyaraka hizo akasema ndizo zenyewe na hivyo tukaendelea na kikao,” alisema Kilango.
Naye Salehe alisema kuwa wajumbe wake hawakupata nyaraka hizo na kwamba amewaelekeza utaratibu wa kuziomba kwa katibu wa Bunge Maalumu.
Tatizo la kukosekana kwa nyaraka lilitokea hata kwa wajumbe wa kamati namba mbili inayoongozwa na Shamsi Vuai Nahodha.
Mwenyekiti wa kamati namba tano, Hamad Rashid Mohammed, alisema kuwa mambo yalikwenda vema kwa wajumbe wake ambao aliwasifu kuwa walijibishana kwa hoja.
Licha ya wenyeviti kusema kwamba mijadala ilikwenda vizuri bila vurugu wala maneno makali, baadhi ya wajumbe walidokeza kuwa mivutano ilijitokeza katika kamati nyingi kati ya wajumbe wa CCM na upinzani kuhusu muundo wa Muungano.
Vyanzo vyetu vilidai kuwa wajumbe wa CCM walikuwa wakisimamia waraka wao unaotaka serikali mbili bila ya kujenga hoja za kushawishi jinsi wanavyotaka kuboresha muundo huo.
Kuhusu kuwepo kwa waraka wa siri badala ya rasimu ya tume, wenyeviti kadhaa waliohojiwa walisema hayo yalikuwa mawazo ya wajumbe binafsi na kwamba kilichokuwa mezani ni rasimu pekee.
Walisema kuwa wajumbe waliruhusiwa kuleta majedwali ya marekebisho ambayo yatapokelewa na kujadiliwa kisha kamati kupiga kura ya ama kuyakubali au kuyakataa.
Hata hivyo, katika kujadili sura ya kwanza yenye sehemu mbili zinazohusu jina, mipaka, alama, lugha na tunu za taifa pamoja na mamlaka ya nchi na utii na hifadhi ya katiba, wapo wajumbe ambao hawakuelewa maana ya nchi, dola huru, serikali na shirikisho. Kwa sababu hiyo, bado wanahitaji ufafanuzi wa kitaalamu.
Kutokana na mkanganyiko huo, wenyeviti wa kamati walisema kuwa wamemwandikia barua Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, ili awapatie wataalamu wa kutoa tafsiri hizo.
Baadhi yao pia wamelalamika kuwa muda wa siku mbili uliotengwa kwa ajili ya kujadili sura mbili kwa kila kamati hautoshi. Wenyeviti wote walisema watamwandikia Sitta kuomba nyongeza ya siku mbili zaidi.
Baadhi ya wenyeviti waliozungumza na vyombo vya habari, walisema kuwa hadi mapumziko ya mchana jana saa 7:00, walikuwa wamejadili sura moja ya kwanza, tena sehemu ya kwanza.
Walisema kuwa hata kufikia siku ya pili leo ambayo ni ya mwisho kwa mujibu wa kanuni, hawawezi kuwa wamegusa sura ya sita. Hivyo wameshauri kanuni hizo zirekebishwe ili kuongeza siku.
CCM wasalitiana
Wakati CCM ikiweka msimamo wa serikali mbili kwa wajumbe wake, baadhi yao wamegeuka na kutetea muundo wa serikali tatu unaopendekezwa kwenye rasimu.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, baadhi ya makada wa CCM (majina yanahifadhiwa) wa Bara na Visiwani jana waligomea maagizo ya chama chao, wakaungana na wenzao wachache kama James Lembeli, Kangi Lugola na Deo Filikunjombe ambao tayari wamejipambanua kupigania serikali tatu.
Imebainika kwamba baadhi ya wajumbe waliokaririshwa na kuandikiwa hoja na viongozi wao, wanashindwa kuzijengea uhalali kwa vile, si zao na hazina takwimu.
Tangu kuwasilishwa kwa rasimu ya katiba chini ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, zimekuwepo mbinu za kila aina za kuwalainisha wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waunge mkono serikali mbili.
Aliyeanza mkakati huo waziwazi ni Rais Jakaya Kikwete wakati wa kulizindua Bunge hilo alipowatisha wajumbe kwamba wakipitisha serikali tatu iko hatari ya serikali za washirika kupinduliwa na jeshi.
Pia alisema rais wa serikali hiyo hana mamlaka ya kiuchumi kwa sababu hana ardhi, rasilimali wala dhamana za kukopa kwa ajili ya maendeleo, kisha akataka wachanganye akili zao na zile za kuambiwa.
Tanzania Daima
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top