Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
MSAJILI
wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema hana haja ya
kuhangaika na tuhuma zilizotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kuwa ofisi yake inatumiwa ili kukisambaratisha chama hicho.
Amewataka Watanzania watulie na ukweli utabainika tu, ikizingatiwa siku za mwizi ni arobaini.
Jaji Mutungi alisema hayo jana, alipozungumza na MTANZANIA kuhusu tuhuma zilizoelekezwa katika ofisi yake na Chadema.(Martha Magessa)
"Anayesema
ofisi yangu inatumika tumwache aseme lakini 'data na facts' zitaeleza
ukweli... mwizi mpe siku arobaini utambaini. Nasikitika na wanaosema
hivyo, lakini katika mpira na siasa haya yapo.
"Sisi bwana ni kama refa, tukiletewa kitu tunashughulikia. Wanachama wanaotaka kujua ukweli watajua tu," alisema Jaji Mutungi.
Jaji
Mutungi ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku mbili baada ya Chadema kumtaka
ajitokeze hadharani kubainisha ukweli iwapo yeye ndiye aliyemtuma
msaidizi wake, Sisty Nyahoza kusema kuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe, hana sifa ya kugombea uongozi ndani ya chama hicho kutokana na
kuzuiwa na Katiba ya Chadema.
Nyahoza
alikaririwa na vyombo vya habari hivi karibuni akisema Mbowe hana sifa
za kugombea uongozi wa chama hicho, kwa vile katiba ya chama hicho
inambana.
Alisema kipengele cha ukomo wa mgombea katika katiba Chadema ya mwaka 2006 kiliondolewa kinyemela bila idhini ya mkutano mkuu.
Nyahoza
alisema katiba ya Chadema ya mwaka 2004 ilikuwa na kipengele cha ukomo
wa madaraka kilichoeleza kuwa kiongozi aliyeongoza vipindi viwili vya
miaka mitano mitano hawezi kuwania tena nafasi hiyo.
Mvutano huo ulikifanya chama hicho kumlaumu Msajili, Jaji Mutungi, kikidai ofisi yake inatumiwa na wasaliti wa chama hicho.
Julai
mosi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alisema
Jaji Mutungi hana mamlaka ya kubaini sifa za viongozi wa chama hicho,
bali wenye mamlaka hayo ni wanachama wa chama hicho pekee.
Mnyika
alisema mwaka 2006, katiba ya Chadema haikurekebishwa, bali iliundwa
upya na kuridhiwa na mkutano mkuu wa chama na kwamba Agosti 13, 2006
ilizinduliwa na nyaraka zote alikabidhiwa Msajili wa Vyama wa wakati
huo, John Tendwa.
Alisema
katika mchakato huo yalikuwapo mabishano na makubaliano katika baadhi ya
masuala, lakini suala la ukomo wa uongozi liliafikiwa na wanachama wote
bila tatizo na kupitishwa kuingizwa katika katiba na Ofisi ya Msajili
ilipelekewa fomu ya marekebisho na katiba mpya kama sheria inavyotaka.
"Tunachomtaka
Mutungi ni kuheshimu katiba ya chama na kuwaheshimu wanachama wa
Chadema na ayapuuze madai ya wasaliti wachache. Kama vipi asubiri aone
uamuzi wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu ubainishe kama katiba ilivunjwa,"
alisema Mnyika.
CHANZO:MTANZANIA
Post a Comment