Naibu Kamishna uhamiaji mkoa wa Njombe Bi. Rose Mhagama akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake.
Baadhi ya wakazi wa mjini Makambako Mkoani Njombe waliojitikeza
kuwaangalia wahamiaji hao( kulia) na waliokaa ni raia wa Ethiopia mara
baada ya kukamatwa na kufikishwa katika ofisi za uhamiaji za Makambako.
Na James Festo, Njombe.
IDARA
ya Uhamiaji Mkoani Njombe, imefanikiwa kuwanasa wahamiaji haramu 21
walioingia nchini kwa kutumia roli la kubebea mifuko ya saruji ambalo
lilikamatwa na maofisa uhamiaji katika eneo Mashujaa kwenye Halmashauri
ya Mji wa Makambako.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake, Naibu Kamishna wa Idara ya
Uhamiaji Mkoani Njombe, Rose Mhagama alithibitisha kukamatwa na
kushikiliwa kwenye kituo cha polisi Makambako wahamiaji hao ambao ni
raia wa kutoka nchini Ethiopia.
Mhagama
alisema askari wa kikosi cha uhamiaji mnamo Agosti 14,mwaka huu majira
ya saa 12:30 jioni wakiwa kwenye doria katika barabara kuu ya kutoka
Makambako kwenda Songea walilishuku na kulisimamisha roli namba T587 CSN
likiwa na tela namba T780 CHM lililokuwa likiendeshwa na dereva
aliyefahamika kwa jina moja la Nyange na kuanza kulikagua.
Pasipoti Nne za Baadhi ya Wahamiaji Hao Waliokamatwa Mjini Makambako
Alisema
roli hilo aina ya IVECO mali ya Everest Flight LTD, S.L.P 77004 DSM
baada ya dereva huyo kusimamisha, askari hao walianza ukaguzi kwenye
gari hilo, na baadaye walibaini kulikuwa na watu kadhaa wamefichwa.
Kufuatia
kubaini kuwepo kwa watu hao, dereva wa roli hilo alipohojiwa alikiri
kubeba watu hao, na kuwaeleza askari Uhamiaji kuwa alikuwa
akiwasafirisha kwenda nchini Malawi kupitia mkoani Ruvuma.
"Dereva
alipohojiwa alisema alikuwa anakwenda kukutana na mtu ambaye anahusika
na watu hao akiwa mjini Njombe, ili aweze kuwashusha pale Njombe na
waweze kuendelea na utaratibu wao walioupanga wa kwenda nchini Malawi,"
alisema Mhagama.
Naibu
Kamishna huyo wa Uhamiaji alisema baada ya kuendelea kufanya upekuzi,
askari wa uhamiaji waligundua kuwepo na watu 10 waliokuwa wamefichwa
kwenye mifuko hiyo ya saruji, na ndipo dereva huyo aliamuliwa kulipeleka
lori hilo kituoni.
"Baada
ya kufika kituoni, askari wakiwa wanaendelea kuwashusha watu hao idadi
yao iliongezeka na kufikia 21, dereva wa roli hilo alifanikiwa kutoroka
na kwamba jeshi la polisi linaendelea kumsaka ili aweze kufikishwa
mahakamani," alisema Mhagama.
Mhagama
alisema kufuatia kukamatwa kwa wahamiaji hao, walipohojiwa walisema
wameingia nchini wakitokea Mombasa nchini Kenya kupitia mkoani Tanga na
kwamba walikuwa wakielekea nchini Malawi.
Orodha ya majina ya wahamiaji hao.
Naibu
Kamishna huyo wa Uhamiaji alitoa mwito kwa raia wema mkoani hapa
kuendelea kutoa ushirikiano wa kuwafichua wahamiaji haramu wanaoingia
nchini kupitia njia za panya. Alisema kuanzia kipindi cha Januari hadi
Agosti, mwaka huu jumla wa hamiaji 25 walikamatwa na kuhukumiwa vifungo
vya, ambapo wahamiaji 24 walikuwa ni kutoka nchini Ethiopia na raia
mmoja alikuwa akitoka nchini Congo.
Wakati
huo huo, Mnadhimu wa jeshi la Polisi mkoani Njombe, SSP Yahaya Rajabu
alithibitisha kukamatwa na kushikiriwa kwa wahamiaji hao 21 kutoka
Ethiopia.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Rajabu alisema wahamiaji hao walikamatwa katika
mtaa na kata ya Mjimwema uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Makambako
majira ya saa mbili usiku.
Post a Comment