Kepteni Mstaafu Alhaji Mohamed Ligora (katikati) akisisitiza
umuhimu wa kupata Katiba bora ya nchi wakati akizungumza na waandishi
wa habari leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mzee Sheikh Yahaya Ngoma
na kulia ni Mzee Alhaji Sheikh Bakari Chiwaka.
Kepteni
Mstaafu Alhaji Mohamed Ligora akisisitiza (katikati) umuhimu wa kupata
Katiba bora ya nchi wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini
Dar es salaam. Kushoto ni Mzee Sheikh Yahaya Ngoma na kulia ni Mzee
Alhaji Sheikh Bakari Chiwaka.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Assah Mwambene akiwasikiliza
Wazee wa mkoa wa Dar es salaam mara baada ya mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam. Picha zote na Eleuteri Mangi-MAELEZO
****************************************************
Na Immaculate Makilika –MAELEZO_DAR ES SALAAM
WAZEE wa
Mkoa wa Dar es salaam wamewaomba Umoja wa Katiba wa Wananchi (UKAWA)
kurudi Bungeni ili kuendelea na mchakato wa majadiliano ya Rasimu ya
Katiba Mpya yanayoendelea.
Wazee
hao wamesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wakizungumza na
waandishi wa habari kuhusu hali ya siasa nchini pamoja na Bunge la
Katiba Mpya linaloendelea mjini Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya Wazee wenzake Kepteni Mstaafu Alhaji Mohamedi Ligora , amesema kuwa Tanzania ni nchi nzuri na watu wake ni wazuri ni vema UKAWA na wenzao wakarudi Bungeni kujadiliana ili watimize matakwa ya kidemokrasia.
Amesema kuwa wananchi wa Tanzania hawataki kufananishwa na
nchi zingine zilizofanya makosa na kupata matatizo kutokana na mambo
kama haya ambayo yalisababisha wananchi wao kuzikimbia nchi zao kwa
mambo ambayo wangeweza kukaa chini na kumaliza wenyewe kwa ajili ya
maslahi ya umma.
Kapteni Mstaafu Alhaji Ligora amesema kuwa suala la mchakato ni suala la kidemokrasia, hivyo ni vyema UKAWA
wakatumia fursa hiyo waliyonayo kwa kurudi Bungeni na kuendelea na
majadiliano kuhusu Rasimu ya Katiba hali itakayosaidia kupatikana kwa
Katiba Mpya ambayo itakuwa na manufaa kwa wananchi wa Tanzania.
Aidha,
amewaomba wajumbe walio Bungeni na wale walio nje ya Bunge kuacha
kuwazomea UKAWA badala yake wawasihi warudi katika chombo rasmi cha
kuboresha Rasimu ya Katiba Mpya.
Naye Mzee Ali Bakari Muki, amewataka UKAWA kuheshimu misingi ya demokrasia lakini pia amewapongeza wabunge walioitikia wito wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa
kurudi Bungeni na kuendelea na majadiliano kuhusu Katiba kwani ndio
Jukwaa pekee la kuwapatia wananchi Katiba bora.
Kwa upande wake Mzee Yahaya Ngoma amewataka viongozi wote hasa UKAWA kuheshimu na kudumisha jitihada zilizofanywa na waasisi
wa Taifa hili akiwemo Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere
pamoja na Sheikh Abeid Amani Karume kwa kuzingatia misingi na kanuni za
uongozi bora kwa kutumia njia ya majadiliano pale panapokuwa na mawazo tofauti baina yao.
Halikadhalika, Alhaji Sheikh Bakari Chikawa amempongeza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa
kuridhia kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya na kusisitiza ni moja ya
tunda la uongozi bora na demokrasia nchini.
Aidha,
ameongeza kuwa UKAWA ni vema wakatumia fursa hiyo ya demokrasia kwa
kuwawakilisha vema wananchi wa Tanzania ili kuhakikisha wanapata Katiba
Bora.
Alhaji Chikawa amewaomba UKAWA
kurudi Bungeni kwani kunyume na hivyo ni watakua wametenda dhambi na
madhara yake ni makubwa sana, na kusisitiza kuwa mazungumzo ni muhimu na yakipuuzwa basi kuna madhara.
Post a Comment