CHAMA Cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), Wilaya ya Mtwara Mjini,
jana walishindwa kuandamana baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa,
kuwashikilia viongozi wa chama hicho kuanzia saa moja asubuhi hadi sita
mchana.
Maandamano hayo yalitarajiwa kufanyika kuanzia maeneo ya Makanaledi
kupitia Mnarani, barabara ya Zambia, Stendi Kuu, Madukani, Bima, Coco
Beach hadi viwanja vya Mashujaa, ambako wangezungumza na wananchi,
lakini yalidhibitiwa na polisi ambao walionekana wakirandaranda kila
kona pamoja na magari ya JWTZ kuhakikisha hakuna maandamano hayo.
Viongozi walioshikikiwa na polisi ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema
Wilaya ya Mtwara Mjini, Ibrahimu Mandoa, Mkufunzi Chadema Mkoa, Ismail
Liuyo, Katibu Stanslaus Sumi na Katibu Mwenezi Hassani Mbangile.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kutoka kituo cha
Polisi Wilaya, Mwenyekiti huyo wa Wilaya, Ibrahimu Mandoa, alisema jana
Chadema Wilaya walikusudia kufanya maandamano ya amani katika Manispaa
ya Mtwara-Mikindani kupinga kuendelea kwa Bunge maalum la Katiba
linaloendelea Dodoma.
Alisema kuwa, kimsingi kila mtu atakuwa anaelewa kuwa Rais Kikwete na
vyama vya siasa ambavyo viko chini ya TCD, walikuwabaliana kwa pamoja
kwamba hakuna uwezekano wa kuweza kupatikana Katiba mpya sasa hivi mpaka
2016 ndio zoezi la mchakato mzima liendelee.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Augustine Ollomi,
alithibitisha kukamatwa kwa viongozi hao na kuhojiwa kwa sababu ya
kusambaza vipeperushi kwa wananchi.
Ollomi, alisema kuwa viongozi wa Chadema walitoa taarifa ya kufanya
mkutano Septemba 21, lakini Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Andrew
Ndassa, aliwakatalia kwa sababu zilizotolewa zilikuwa kinyume, wao
walitaka kufanya mkutano kupinga Bunge maalumu ambalo linaendelea
Dodoma, na kwa ufahamu wake bunge hilo liko kisheria sio kama wanavyodai
Chadema.
Alisema, juzi walipata vipeperushi ambavyo vilikuwa vimeandaliwa na
viongozi Chadema mkoani hapa wakiwashawishi wananchi washiriki katika
maandamano, hivyo ndio sababu ya kuwaita kwa ajili ya mahojiano.
Post a Comment