BAADA ya ndoto ya kuziunganisha pande
mbili za katikati ya Jiji la Dar es Salaam na Kigamboni kwa daraja lenye
umbali wa meta 680, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)
linaangalia uwezekano wa kujenga daraja la kihistoria zaidi
litakalounganisha Dar es Salaam na Zanzibar.
Kwa sasa, uongozi wa shirika hilo upo
katika mazungumzo na wataalamu mbalimbali ili kuangalia uwezekano wa
kujenga daraja hilo katika bandari ya Dar es Salaam kwa upande wa
Tanzania Bara na Unguja, kwa upande wa Zanzibar.
Umbali kati ya Dar es Salaam na Zanzibar
ni kilometa 73.43, sawa na maili 45.62 hivyo kuwapo kwa mradi huo ni
jambo linalowezekana, kwani kuna madaraja marefu zaidi duniani
yanayounganisha upande mmoja wa bahari na mwingine.
Kwa sasa, daraja refu kabisa duniani ni
lile la Danyang–Kunshan lililopo China ambalo lina umbali wa kilometa
165, sawa na maili 102.4. Daraja hilo lilifunguliwa Juni mwaka 2011.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa
NSSF, Dk Ramadhan Dau wakati alipokuwa akijibu swali la Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda ambaye
alitaka kufahamu kama kuna matarajio ya kujenga daraja kubwa zaidi,
ikiwezekana la kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Alisema wapo katika mazungumzo na
wataalamu mbalimbali ambapo mazungumzo hayo yakienda sawa, ujenzi wa
daraja hilo huenda isiwe ndoto, bali ukweli.
"Hilo wazo lipo mheshimiwa na tayari
tumeshaanza mazungumzo ya awali, kwa hiyo hilo wazo lipo na sisi
tulilifikiria," alisema Dk Dau.
Kamati hiyo ilifanya ziara katika miradi
mikubwa mitatu ya shirika hilo ambayo ni daraja la Kigamboni, ujenzi wa
nyumba za Mtoni Kijichi na 'Dege Eco village' ambao una nyumba zaidi ya
7,000.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara
hiyo, Mtanda alisema, kamati yake imeridhishwa na miradi hiyo ya NSSF
ambayo inaendelea huku akitaka kuongezwa kwa kasi ili watanzania waanze
kunufaika na miradi hiyo.
"Muangalie na hilo la ujenzi wa daraja
la kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar na mradi wa makazi bora na salama
ambao utaweza kubadili taswira ya Jiji la Dar es salaam," alisema.
Alisema kamati yake isingependa kuona
changamoto zozote ambazo zinaweza kukwamisha miradi hiyo na kwamba
serikali kupitia Wizara ya Ujenzi itaangalia namna ya kuunganisha
miundombinu karibu na miradi hiyo.
"Lakini pia tumesikia kuwa serikali
inadaiwa na mifuko ya hifadhi, tunashauri serikali kuilipa mifuko hii
ili kuifanya kuwa na nguvu na kuweza kuleta maendeleo," alisisitiza
Mtanda.
SOURCE: HABARI LEO
Post a Comment