Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania
(TWPG) wajivunia manufaa waliyopata wanawake katika Rasimu ya mwisho ya Katiba
inayopendekezwa.
Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM.
Wabunge Wanawake nchini wamekuwa Wanaharakati wakubwa
wenye kudai haki za wanawake za jinsia kila kukicha hasa kupitia mchakato wa
kusaka Katiba mpya ambapo hivi karibuni wamefanikiwa katika kuhakikisha kuwa madai
yao yanasikilizwa na kuwekwa katika Katiba mpya ijayo kutokana na ukweli
kwamba, Rasimu ya mwisho ya Katiba inayopendekezwa imefanikiwa kuyaingiza madai
mbalimbali yanayohusu masuala ya kijinsia kwa wanawake.
Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG) hawanabudi
kupongezwa kwa kazi kubwa walioifanya katika kuhamasisha umma na wajumbe
wengine wa Bunge Maalum juu ya haki sawa ya jinsia ya hamsini kwa hamsini kwa
hatua kubwa waliyofikia na manufaa waliyoyapata wanawake katika Rasimu hiyo.
Hivi karibuni, Umoja huo wa Wabunge Wanawake walifanya
semina iliyohusu kwa ajili ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuhusu masuala
ya maandiko ya Kisera na manufaa waliyopata wanawake katika Rasimu hiyo ya
mwisho inayopendekezwa huku wajumbe hao wakichangia mada mbalimbali kuhusu
mafanikio yao na furaha yao ya kuona kuwa wamepiga hatua nzuri katika kudai
haki zao za Kikatiba.
Akitoa mada wakati wa Semina hiyo, Katibu Mkuu wa TWPG
ambaye pia ni Mjumbe wa bunge hilo, Mhe. Angellah Kairuki alisema kuwa moja ya
manufaa ambayo wanawake watayapata katika Katiba mpya ijayo ni kuhusu masuala
ya Uongozi ulio bora wenye kuzingatia sifa na weledi katika michakato ya ajira
na uteuzi ambapo suala hilo limetiliwa nguvu katika Ibara ya 208, Ibara ndogo
ya kwanza kipengele C ambapo katika masuala ya uteuzi na mambo ya ajira katika
nafasi mbalimbali katika Utumishi wa Umma utazingatia uwezo wa kitaaluma,
weledi, ujuzi, usawa wa jinsia hivyo suala la usawa wa jinsia limezingatiwa.
Mhe. Kairuki alieleza kuwa, Sura ya Kumi ya Rasimu ya
mwisho ya Katiba inayohusu masuala ya Bunge kama ilivyoelezwa katika Ibara ya
129 ibara ndogo ya Nne, inaeleza kuwa, kwa kutambua kuwa Bunge ndiyo mhimili
muhimu wa dola, Katiba inayopendekezwa imekusudia kurekebisha kasoro iliyopo ya
uwakilishi mdogo wa wanawake bungeni ambapo hivi sasa kuna asilimia 36.6% ya
wanawake bungeni.
“Kupitia Katiba hii inayopendekezwa kupitia Ibara ya 129
Ibara ndogo ya Nne tutakuwa na uwakilishi uliosawa baina ya Wabunge Wanawake na
Wabunge Wanaume”, alisema Mhe. Kairuki.
Aidha, aliwaeleza wajumbe hao kuwa katika Sura ya 12
inayohusu Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Utumishi wa Mahakama
imepewa wajibu katika ajira mbalimbali na uteuzi kuhakikisha kuwa inazingatia
usawa wa jinsia.
Haki mbalimbali za wanawake zinabainishwa katika
baadhi ya Mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo Tanzania imeridhia, na hapa Mhadhiri
Msaidizi wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Iringa, Bw. Dunford Mpelumbe anafafanua
kwamba Mikataba ambayo Tanzania imeridhia pamoja na baadhi ya Itifaki za
Kimataifa yakiwemo maazimio mbalimbali ambayo Tanzania kama Mwanachama wa
Jumuiya ya Kimataifa imeridhia na hatua kubwa iliyopigwa na Serikali katika
kusimamia suala la jinsia na haki za wanawake.
Katika haki za wanawake tunapozitazama kwa jicho la
Kimataifa na tunapokuja ndani ya nchi ni muhimu pia kutunga sheria kwa kuziweka
katika Katiba na ni vema kuunda Taasisi maaalum ambayo itakuwa inasimamia utekelezaji
wa masuala hayo ya wanawake.
Mpelumbe alifafanua kuwa katika Azimio la 1948 (Universal Declaration of Human Rights) katika
Ibara yake ya kwanza inaelezea juu ya mambo ya usawa kati ya mwanamke na
mwanaume, lakini pia suala la usawa kati ya binadamu wote umepewa kipaumbele.
Aidha, aliongeza kuwa, licha ya Mikataba ya Kimataifa
pamoja na Sheria mama zilizopo sasa nchini, haki za wanawake zinatakiwa
kujengewa ulingo wa kuzisemea mara kwa mara ili watu wapate kuzielewa vizuri.
“Nchi za wenzetu wameweka jitihada za dhati kabisa
katika kujenga uwezo wa mwanamke na jitihada hizi zinatokana na utiaji sahihi
na kuridhia hii Mikataba ya Kimataifa mbalimbali ambayo inatoa haki za wanawake
lakini hatua ya pili ni kwa kuchukua hatua za msingi za kikatiba na kisheria
kuziweka hizo haki za mwanamke katika ulingo wa Kimataifa zionekane zaidi na kwa
uwazi kabisa katika Katiba ya nchi na Sheria za nchi”, alisema Mpelumbe.
Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni mjumbe wa Bunge
hilo, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro naye aliwapongeza wajumbe wanawake kwa kuwa na
mshikamano ambao Wabunge wanawake wa Bunge hilo waliuonyesha, na hapa akaeleza
kwamba wajumbe hao waliweza kushikamana kwa kuonyesha kuwa ‘Umoja ni nguvu,
Utengano ni udhaifu’ bila ya kujali Vyama walivyotoka, Kundi waliloliwakilisha,
Sura na hata afya zao wajumbe hao walishakamana katika kuhakikisha kuwa haki
zao zinazingatiwa katika Katiba mpya iyao.
Dkt. Migiro aliendelea kusema kuwa suala la hamsini
kwa hamsini limekaa vema katika Rasimu ya mwisho ya Katiba inayopendekezwa na
itawapa wanawake wengi msingi wa kuteremka chini kwani wanawake wengi wamekuwa
wakijitokeza kwa wingi katika Mabaraza ya Kata na Taasisi zenye mrengo
unaofanana na wamekuwa waaminifu ndani ya Bunge Maalum katika kuhakikisha kuwa
haki zao zinawekwa ndani ya katiba hiyo.
“Katiba hii ni yenu, na tutakwenda kuipigia debe kwani
ni Katiba ambayo imetuweka mahali pazuri kwa kuimarisha haki ndani ya nchi
yetu, maslahi ndani ya taifa letu, kuimarisha Muungano wetu na umoja wetu”,
alisema Dkt. Migiro.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ambaye
pia ni mjumbe wa bunge hilo, Mhe. Sophia Simba nae alieleza juu ya mafanikio
hayo yaliyofikiwa na Umoja huo akisema kuwa licha ya kazi kubwa inayoendelea ya
kuipinga Rasimu ya Katiba inayopendekezwa ambayo hali hiyo inaweza kusababisha
wanawake kukosa haki zao za msingi walizosipigania kuna haja ya wanawake
kujifunga mkanda katika kuhamasisha umma wa Watanzania kuipigia kura ya ndiyo
katika hiyo ili iweze kupita na hatimaye kuwa na Katiba kamili mpya yenye
kujali makundi yote nchini.
Mhe. Simba alisema kuwa TWPG ndiyo wakala ambao
wanaweza kusaidia wanawake katika kuhamasisha umma kwa lengo la kupeleka ujumbe
wa uhamasishaji kuhusu kuipigia kura Rasimu ya mwisho ya Katiba
inayopendekezwa.
“Nyie ndiyo Agency huko mnaoweza kutusaidia, tukitaka
kwenda Vyuoni, kwa Wakulima, kwa Wavuvi, si nyie hapo ndo mtakaotusaidia?!,
kwahiyo kazi haijaisha Aruta continua”, alisisitiza Mhe. Simba.
Mhe. Simba kwa upande mwingine alisistiza juu ya suala
la ushirikiano baina ya wanawake wote nchini na aliwahamasisha wajumbe wenzie
kutilia mkazo suala la kipengele cha kujali haki za watu wenye ulemavu kiweze
kuingizwa katika Katiba mpya ijayo.
Naye mjumbe mwingine wa Bunge hilo toka kundi la 201,
Mhe. Dkt. Avemaria Semakafu alisema kuwa ili kuwezesha kurejesha rasilimali
zilizoko pembezoni ni pamoja na kuzielezea fursa sawa baina ya wanawake na
wanaume ikiwemo usawa wa jinsia, usawa wa kumiliki ardhi, elimu afya na
mengineyo.
Post a Comment