---
Na Felix Mwagara, Nachingwea
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge
wa Jimbo la Nachingwea, Mathias Chikawe ametangaza rasmi kuwa atagombea
tena katika nafasi ya ubunge kupitia CCM katika uchaguzi Mkuu ujao na
kulitetea jimbo lake. Alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na wananchi
pamoja na viongozi wa CCM wa Wilaya na Kata ya Mtua, wilayani Nachingwea
katika sherehe ya kuwapokea viongozi na wanachama wapya wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliojiunga na CCM wilayani humo.
Waziri Chikawe alisema wananchi wake bado wanamuhitaji
kwa hiyo hawezi kuacha kugombea nafasi hiyo kwani wazee na wananchi
mbalimbali katika Kata zote alizokuwa akipita kufanya mazungumzo nao
wanamuomba agombee tena nafasi hiyo.
“Wakati nikiingia ubunge mwaka 2005 katika jimbo
hili kulikuwa hakuna lami na barabara nyingi za kwenda vijijini zilikuwa
hazipitiki na pia maji yalikuwa shida lakini sasa barabara za lami mjini
Nachingwea zimejengwa, maji yanapatikana tena yasio na chumvi, barabara
vijijini zinapitika kwa kuwa zimechongwa vizuri kwa kuwawezesha wakulima
kupitisha mazao yao,” alisema Chikawe huku akishangiliwa na mamia
ya wananchi waliofurika katika sherehe hiyo. Picha/Story na Felix Mwagara.
Post a Comment