KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema vyama vya upinzani vitaendelea kuwa wasindikizaji wa CCM katika chaguzi mbalimbali zitakaofanyika nchini kutokana na wananchi wengi kuendelea kukiamini chama hicho.
Aidha amesisitiza kuwa Katiba Inayopendekezwa itapita
kwa kishindo wakati wa Kura ya Maoni itakayofanyika Aprili 30, mwaka huu, pamoja
na kelele na shinikizo la vyama vya upinzani kutaka wananchi kususia upigaji
kura wa Katiba hiyo.
Nape aliyasema hayo katika maeneo mbalimbali ya wilaya
ya Chamwino, wakati Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alipofanya ziara
wilayani humo katika mwendelezo wa ziara yake ya kuutembelea Mkoa wa
Dodoma.
Akizungumzia ushindi wa chama hicho katika uchaguzi
mkuu ujao wa udiwani, ubunge na urais, Nape alisema hakuna siri kuwa vyama vya
upinzani vitaendelea kuisindikiza CCM ili kushinda viti vingi vya udiwani,
ubunge na kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi wa urais.
“Ndugu zangu nataka niwaeleze wazi kwamba vyama vya
upinzani ni kama mpambe wa Bwana Harusi, ambaye pamoja na kufanya shughuli zote
za usaidizi na upambe kwa Bwana Harusi lakini safari yake huishia sebule
maharusi wanapofika nyumbani,” alisema Nape.
Alisema tayari ishara ya ushindi wa CCM imeonekana
katika uchaguzi wa serikali za mitaa, ambapo CCM imeshinda kwa kishindo kwa
kunyakua viti vingi kwenye vitongoji, mitaa na vijiji, huku vyama vya upinzani
vikiambulia ushindi katika baadhi ya maeneo.
“Nataka niwaambie wazi, wananchi wa nchi hii bado
wana imani kubwa na CCM, ukiona kuna mtu anakipenda chama cha upinzani ujue
anasumbuliwa na ushamba tu na si kitu kingine. Sisi tumezunguka nchi nzima na
tumegundua wakati CCM inazidi kuimarika na kupanda juu, vyama vya upinzani
vinazorota na kushuka chini, wenye macho na walione hili,” alisena
Nape.
Post a Comment