Mkurugenzi wa Sensa na
Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa
taarifa ya kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei nchini kwa mwezi Februari, 2015. Kulia
kwake ni Kaimu Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi hiyo Bi. Ruth Minja.
Baadhi ya Waandishi wa
Habari wakiwa kazini wakati Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim
Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu akizungumza nao leo jijini Dar es
Salaam kuhusu taarifa ya kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei nchini kwa mwezi
Februari, 2015. (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO).
Na Veronica
Kazimoto,
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa
mwezi Februari, 2015 umeongezeka kwa asilimia 4.2 kutoka asilimia 4.0 mwezi
Januari mwaka 2015.
Hayo yamesemwa leo na
Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa
ya Takwimu (NBS) ambapo amesema kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma
kwa mwaka ulioishia mwezi Februari, 2015 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na
kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2015.
“Kuongezeka kwa Mfumuko wa
Bei wa mwezi Februari, 2015 kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya
bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi
Februari, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Februari, 2014, amesema
Kwesigabo”.
Bidhaa za vyakula
zilizoonyesha kuongezeka mwezi Februari, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi
Februari, 2014 ni pamoja na bei za mchele (asilimia 18.5), unga wa mihogo
(asilimia 9.3), nyama (asilimia 8.9), samaki (asilimia 12.4) na maharagwe kwa
asilimia 7.1.
Kwa upande wa bidhaa zisizo
za vyakula zilizoonyesha kuongezeka mwezi Februari, 2015 zikilinganishwa na bei
za mwezi Februari, 2014 ni pamoja na bei za mavazi ya wanaume (asilimia 4.7),
mavazi ya wanawake (asilimia 3.3), mkaa (asilimia 5.1), mashuka (asilimia 3.1)
na gharama za kumuona daktari kwa asilimia 11.2.
Akizungumzia kuhusu Mfumuko
wa Bei kwa kipimo cha mwezi Mkurugenzi Kwesigabo amesema kuwa Mfumuko wa Bei wa
mwezi Februari, 2015 unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 1.6
ukilinganisha na ongezeko la asilimia 1.0 mwezi Januari,
2015.
Aidha, Kwesigabo
amesisitiza kuwa Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi kufikia 154.83 mwezi
Februari, 2015 kutoka 152.43 mwezi Januari, 2015 ambapo kuongezeka kwa fahirisi
kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za
vyakula.
Kwa upande wa thamani ya
shilingi, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo amesema uwezo
wa Shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umefikia Shilingi 64
na senti 59 mwezi Februari, 2015 kutoka mwezi Septemba, 2010 ikilinganishwa na
Shilingi 65 na senti 60 ilivyokuwa mwezi Januari, 2015.
Hata hivyo, Mfumuko wa Bei
nchini Tanzania una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika
Mashariki kwa kuwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Februari, 2015 nchini Uganda
umeongezeka hadi asilimia 1.4 kutoka asilimia 1.3 mwezi Januari, 2015; na nchini
Kenya, Mfumuko wa Bei wa Mwezi Februari, 2015 umeongezeka hadi asilimia 5.61
kutoka asilimia 5.53 mwezi Januari, 2015.
Post a Comment