Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, wametoa salamu za pole na rambirambi kwa wananchi wa kijiji cha Mwakata wilayani Kahama walioathirika na mvua ya mawe na upepo mkali hivi karibuni.
Akizungumza kwa niaba ya Lowassa ambaye pia ni mbunge
wa Monduli, mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga, Hamis
Mgeja, alisema mbunge huyo ametoa rambIrambi ya Sh. milioni tano kwa ajili ya
wananchi wote walioathirika.
“Naungana na wananchi wote kwa kuwapa salamU za pole
na rambirambi baada ya kutokea janga hilokubwa lilipoteza watu wengi na
mali…tupo pamoja katika kipindi hiki cha majonzi,” alisema Mgeja kwa niaba
ya Lowassa.
Alisema atazidi kushirikiana na wananchi hao katika
maombi ili wale waliojeruhiwa katika tukio hilo waweze kurejea katika hali yao
ya kawaida.
Lowassa alisema Tanzania ni moja, wananchi wake ni
wamoja hivyo lazima katika kipindi hiki wawe wamoja na kuepukana na minong’ono
yoyote inayoweza kuwatenganisha katika umoja wao.
Mgeja alisema pamoja na kuwapo na maneno maneno awali
kati ya viongozi wa serikali na chama, lakini chama chake hakina matatizo yoyote
kwa sasa kutokana na serikali kuanza kutimiza majukumu yake.
“Chama hakina matatizo na serikali ya mkoa ama
wilaya, lakini ilikuwa ni kukumbushana kuwatumikia wananchi hawa kipindi
walichopatwa na janga lile…tushirikiane ili kurejesha hali nzuri kwa watu
hawa,” alisema Mgeja.
Naye mwenyekiti wa Chadema, Mbowe, alisema chama chake
kinaungana na Watanzania wote katika kuomboleza janga hilo lililoathiri watu
wengi katika kijiji cha Mwakata.
“Tusiingize siasa katika jambo hili bali
tunachotakiwa tuungane wote huku serikali ikiwa na jukumu la kuhakikisha ina
wajibu wa kuwahudumia watu hawa,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema chama chake kinatoa rambirambi ya
Sh.milioni 10 kwa ajili ya waathirika hao, lakini alimuomba mkuu wa mkoa wa
Shinyanga, Allynassoro Rufunga, pesa hizo aseme wanunue mahitaji
gani.
“Kiasi hiki hatuwezi kutoa taslim, bali tunaomba
tuelezwe tununue mahitaji yapi ili yawanufaishe wananchi hawa walioathirika na
mvua ya mawe na upepo mkali,” alisema.
Aidha, Mbowe alimpa pole mbunge wa jimbo la Msalala,
Ezekiel Maige, kutokana na janga hilo kutokana na kutokea ndani ya jimbo
lake.
Mkuu wa wilaya ya Kahama, Mpesya, alimshukuru Mbowe kwa
niaba ya chama chake kwa kuonyesha ubinadamu kuweza kuwasaidia waathirika
hao.
“Hapa hakuna siasa, bali janga hili ni la kila
mmoja…Chadema wameonyesha mfano na kuona hakuna itikadi katika majanga,
tushirikiane kwa pamoja mheshimiwa Mbowe,” alisema
Mpesya.
Naye mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga,
aliwashukuru wote waliochangia waathirika hao akiwamo Lowassa na Chadema, huku
akimuomba mwenyekiti Mbowe pesa walizotoa wanunulie mabati pamoja na
maturubai.
Post a Comment