Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imeanza mchakato wa mapitio ya viwango vya nauli za mabasi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya
Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, mapitio hayo yana lengo la kubaini haja ya
kurekebisha viwango vya nauli za mabasi hapa nchini.
“ Kwa mujibu wa Sheria ya Sumatra ya 2001 na Kanuni
zake, Mamlaka imeamua kufanya mapitio ya viwango vya juu vya nauli nchini kwa
lengo la kubaini haja ya kufanya marekebisho. Ili kutumiza hili mamlaka
inatakiwa kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufikia uamuzi wa kuridhia viwango
vya tozo kwa huduma zinazodhibitishwa na mamlaka zikiwemo nauli za
mabasi.”
SUMATRA imeandaa mikutano ya kupokea maoni ya wadau wa
usafiri ikiwa ni pamoja na watoa huduma, watumiaji wa huduma na wananchi kwa
ujumla.
Taarifa hiyo inaonesha ratiba ya mikutano ambapo
mkutano wa kwanza umepanga kufanyika Jumatatu ijayo katika Ukumbi wa Gold Crest
Hotel, utafuatiwa na mkutano wa Machi 12 utakaofanyika ukumbi wa NSSF mkoani
Kigoma na wa tatu utafanyika jijini Dar es Salaam Machi 18 katika ukumbi wa
Karimjee.
Akizungumzia hilo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Kutetea
Abiria (CHAKUA), Godwini Ntongeji alisema awali waliiandikia SUMATRA kutaka
washushe bei ya nauli ili wananchi waweze kunufaika na kushuka kwa bei ya mafuta
iliyoanza kushuka kuanzia Januari mwaka huu.
“Awali tuliwaandikia barua SUMATRA, hawakutujibu,
baada ya muda tukawaandikia barua ya kuwakumbusha na ndipo walipotujibu na
tunashukuru tumeshaona matangazo ya kuwaita wadau katika kujadili nauli,”
alisema.
Post a Comment