Mkurugenzi
wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Morrice Oyuke
akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam wakati
akitangaza matokeo ya takwimu za Pato la Taifa kwa robo mwaka ya kwanza
kuanzia mwezi Januari – Machi, 2015 ambayo yameonyesha kuwa thamani ya
Pato la imekua na kufikia shilingi trilioni 21.9 ikilinganishwa na
shilingi trilioni 18.6 ya robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2014.
Baadhi ya
waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi
kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Morrice Oyuke wakati akitangaza matokeo
ya takwimu za Pato la Taifa kwa robo mwaka ya kwanza kuanzia mwezi
Januari – Machi, 2015 ambayo yameonyesha kuwa thamani ya Pato la imekua
na kufikia shilingi trilioni 21.9 ikilinganishwa na shilingi trilioni
18.6 ya robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2014.
Matokeo
ya takwimu za Pato la Taifa kwa robo mwaka ya kwanza yaani kuanzia mwezi
Januari – Machi, 2015 yameonyesha kuwa thamani ya Pato la Taifa imekua
na kufikia shilingi trilioni 21.9 ikilinganishwa na shilingi trilioni
18.6 ya robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2014.(VICTOR)
Akizungumza
na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Takwimu
za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Morrice Oyuke amesema takwimu
hizo zimetayarishwa kwa kuzingatia marekebisho ya Takwimu za Pato la
Taifa kwa bei za mwaka 2007.
“Pato la
Taifa kwa bei za mwaka 2007 katika kipindi cha robo mwaka ya kwanza
linaonyesha kuwa na jumla ya thamani ya shilingi trilioni 10.6 kwa mwaka
2015 ikilinganishwa na shilingi trilioni 9.9 katika kipindi kama hicho
mwaka 2014”, amefafanua Oyuke.
Oyuke
amesema kuwa, Pato hili la Taifa limeongezeka kwa kasi ya asilimia 6.5
katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi
ya asilimia 8.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2014.
Aidha,
Oyuke amesisitiza kuwa utayarishaji wa takwimu za Pato la Taifa
hujumuisha shughuli zote za kiuchumi na hivyo hutumika katika
kutathmini, kupanga mipango na kutayarisha sera za kiuchumi.
Baadhi ya
shughuli hizo za uchumi ni kilimo na mifugo ambazo zilikua kwa kasi ya
asilimia 2.6 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015
ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 3.4 katika kipindi kama
hicho mwaka 2014.
Shughuli
za Uvuvi ziliongezeka kwa asilimia 0.9 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2015
ikilinganishwa na asilimia 2.3 kipindi kama hicho mwaka 2014. Ukuaji huu
ulitokana na jitihada za Serikali kuwasaidia wakulima kwa kutoa ruzuku
na maelekezo ya Ma-ofisa Ugani kwa wakulima kama vile kuchagua mbegu
bora yaliyosaidia kuongeza uzalishaji.
Shughuli
za Uchimbaji Madini, Mawe na Kokoto ziliongezeka kwa kasi ya asilimia
0.6 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na
kasi ya ukuaji wa asilimia 19.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2014.
Shughuli
za Uzalishaji bidhaa Viwandani zilikua kwa kasi ya asilimia 5.7 katika
kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya
asilimia 8.2 kipindi kama hicho mwaka mwaka 2014. Kasi ya ukuaji
ilitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa za vyakula, vinywaji,
tumbaku, nguo, simenti na bidhaa za kemikali na madawa.
Shughuli
nyingine ni pamoja na Uzalishaji nishati ya umeme na maji ambazo zilikua
kwa kasi ya asilimia 10.7 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka
2015 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 10.1 katika kipindi kama hicho
mwaka 2014. Kuongezeka kwa ukuaji wa nishati ya umeme kulitokana na
kuongezeka kwa umeme uliozalishwa kutoka kwenye mitambo inayotumia,
maji, mafuta na gesi asilia.
Shughuli
za Fedha na Bima katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015
ziliongezeka kwa asilimia 9.1 ikilinganishwa na asilimia 11.2 kipindi
kama hicho mwaka 2014.
Shughuli
za Ujenzi (ambazo zinajumuisha ujenzi wa nyumba za makazi na zisizo za
makazi; barabara na madaraja; na shughuli nyingine za uhandisi) katika
kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ziliongezeka kwa asilimia 8.8
ikilinganishwa na asilimia 21.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2014.
Ofisi ya
Taifa ya Takwimu ina jukumu la kutayarisha na kusambaza takwimu rasmi
nchini ikiwa ni pamoja na takwimu za Pato la Taifa kwa robo Mwaka ambazo
hupimwa kwa kuangalia thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa nchini
katika vipindi vya miezi mitatu mitatu ambavyo ni Januari – Machi,
Aprili – Juni, Julai – Septemba na Oktoba – Desemba.
Post a Comment