Viongozi
wa Marekani wamemwagia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete (pichani) sifa kubwa za ujenzi na ulezi
wa demokrasia, heshima kwa haki za binadamu na zaidi ya yote uheshimu
wa Katiba ambao unamwezesha kuondoka madarakani kwa mujibu wa Katiba ya
Tanzania na kukabidhi madaraka kwa Rais ajaye kwa hiari na kwa amani.
Rais
Kikwete amemwagiwa sifa hizo, Jumanne, Septemba 22, 2015 katika
mikutano yake mbali mbali na viongozi wa Serikali ya Marekani na wa
taasisi kubwa na muhimu zisizokuwa za Kiserikali nchini humo katika
ziara yake ya siku mbili katika mji mkuu wa Marekani wa Washington, D.C.
Rais
Kikwete ametembelea Washington kutoka mjini New York ambako amemaliza
kuendesha vikao vya Jopo la Watu Mashuhuri Duniani wanaotafuta jinsi
gani dunia inaweza kujikinga vizuri zaidi dhidi ya magonjwa ya milipuko
kufuatia madhara makubwa ya ugonjwa wa Ebola.
Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mheshimiwa Anthony J. Blinken
amemwambia Rais Kikwete kuwa uamuzi wake wa kuheshimu Katiba ya Tanzania
kwa kukabidhi madaraka ya uongozi wa nchi baada ya kumaliza vipindi
viwili vya uongozi wake, unatuma ujumbe mzito, dhahiri na unaosikika
sana katika Bara zima la Afrika na Kanda ambako Tanzania ipo.
“Mafanikio
yako ya uongozi yamekuwa ya kifani kabisa. Hayana mfano katika Afrika
ya leo. Umeacha historia kubwa na ya kudumu (legacy) ya kuheshimu
demokrasia na Katiba ya nchi yako. Umeacha na kutuma ujumbe wa wazi kabisa kwa Bara zima la Afrika na katika ukanda ambako nchi yako ya Tanzania ipo,” amesema
Mheshimiwa Blinken katika mkutano uliofanyika katika Hoteli ya
Ritz-Carlton, Georgetown, ambako Rais Kikwete alikuwa amefikia.
Kabla
ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani mwishoni mwa
mwaka jana, Mheshimiwa Blinken alikuwa Msaidizi wa Rais Barack Obama na
Msaidizi Mkuu wa Baraza la Ushauri wa Usalama la Marekani. Pia amepata
kuwa msaidizi wa ushauri wa usalama wa Makamu wa Rais wa Marekani na pia
amepata kuwa ujumbe kwenye Baraza la Ushauri wa Taifa la Rais Bill
Clinton.
Naye Mheshimiwa Ken Wallack, Rais wa Taasisi ya National Democratic Institute (NDI) ya chama cha siasa cha Democratic amemwambia Rais Kikwete:
“Tuseme
hivi…kwa kutilia maanani yanayotokea katika dunia ambako unaishi na
unatokea, sote tunakushukuru na kukupongeza kwa msimamo wako wa
kuheshimu Katiba ya nchi yako. Unajiunga na kundi la viongozi wa
kuheshimiwa sana katika Bara la Afrika ambao hawakuamini kuwa wao tu
ndio wenye uwezo wa kuongoza.”
Mheshimiwa Balozi Mark Green, Rais wa Taasisi ya International Republican Institute (IRI) ya chama cha siasa cha Republican amemwambia Rais Kikwete, ”unaacha mfano kwetu sisi sote katika kupigania na kulea demokrasia duniani na hasa katika Bara la Afrika.”
Balozi Green amepata kuwa Balozi wa Marekani katika Tanzania wakati wa
kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete na alichangia kwa kiasi kikubwa
jitihada za Serikali ya Rais Kikwete katika nyanja nyingi za maendeleo.
Aliyekuwa
waziri mdogo wa Mambo ya Nje Marekani aliyeshughulikia masuala ya
Afrika, Mheshimiwa Johnnie Carson amemwambia Rais Kikwete: “Kuna
kiwango kikubwa cha heshima kwako katika Marekani kwa jinsi
ulivyoongoza nchi yako na Serikali yako katika miaka 10 iliyopita. Chini
ya uongozi wako, Tanzania imeendelea kuonyesha mfano usiokuwa na kifani
katika ujenzi wa demokrasia na umeheshimu sana Katiba ya nchi yako.
Sisi katika Marekani, tunakupongeza sana.”
Balozi Carson ambaye sasa ni Rais wa Taasisi ya Amani katika Marekani ya United States Institute of Peace amesema kuwa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Kikwete imeendelea kuwa rafiki mkubwa zaidi wa Marekani katika Afrika.
Waheshimiwa
Wallack, Balozi Green na Balozi Carson wamezungumza wakati Rais Kikwete
alipokutana kwa mazungumzo na viongozi wa taasisi za NDI, IRI, Peace Institute na
IFES katika makao makuu ya NDI mjini Washington. Mwenyekiti wa NDI,
Balozi Madeline Albright, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani za zamani
hakuweza kuhudhuria mazungumzo hayo hata kama alituma salamu zake kwa
Rais Kikwete.
Akizungumza
baada ya kutolewa sifa zake za kuheshimu demokrasia na Katiba ya
Tanzania, Rais Kikwete amewaambia viongozi wa taasisi hizo maarufu
duniani: “Nawaheshimu sana wale ambao wanataka kuendelea na
madaraka ya kuongoza nchi zao. Kazi ya urais ni kazi ngumu na mzigo
mkubwa, ukiifanya miaka kumi inatosha.”
Ameongeza: “Isitoshe
katika Tanzania tuna jadi sasa ya kuheshimu Katiba. Unachaguliwa kwa
miaka mitano na ukichaguliwa tena unaongeza mingine mitano. Baada ya
hapo unawapisha watu wengine. Isitoshe ni jambo zuri kupata kiongozi mpya baada ya muda ambaye atakuja na mawazo mapya na aina mpya ya uongozi.”
Rais Kikwete amerejea mjini New York usiku wa leo tayari kuhudhuria shughuli za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (General Assembly) mwaka huu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
23 Septemba, 2015
Post a Comment