Mkazi
wa mjini Moshi, Kyefa Joachim Makundi (33), jana alipandishwa kizimbani
akikabiliwa na mashitaka ya kumtukana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Jakaya Kikwete.
Mbali
na shitaka hilo, mshitakiwa huyo alisomewa shitaka lingine la kumtukana
Ridhiwan Kikwete ambaye ni mtoto wa Rais Kikwete ambaye pia ni Mbunge
wa Chalinze aliyemaliza muda wake.
Mshitakiwa
huyo alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya mkoa
Kilimanjaro, Joachim Tiganga na kusomewa mashitaka hayo na wakili wa
Serikali Kanda ya Moshi, Agatha Pima.
Wakili
Pima alidai mahakamani kuwa Oktoba 17 mwaka huu katika baa ya Harambee
iliyopo katikati ya mji wa Moshi, mshitakiwa alitumia lugha ya matusi
dhidi ya Rais Kikwete na mwanae Ridhiwan.
Ingawa
matusi hayo hayakuandikwa kwenye hati ya mashitaka, lakini wakili Pima
alidai kitendo hicho ni kinyume cha kifungu 89(1) (a) cha kanuni ya
adhabu kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Chini
ya kifungu hicho, mtu yeyote anayetumia lugha ya matusi, kuudhi, au
kudhalilisha dhidi ya mtu mwingine katika hali ambayo inaweza
kusababisha uvunjifu wa amani anatenda kosa la jinai.
Adhabu inayotolewa kwa mtu anayepatikana na hatia katika kosa hilo ni kifungo cha miezi sita jela.
Hata
hivyo, mshitakiwa alikana shitaka hilo ambapo mahakama ilisema dhamana
ilikuwa wazi ikiwa mshitakiwa atakuwa na wadhamini wawili watakaosaini
hati ya dhamana ya Sh1.5 milioni kila mmoja.
Post a Comment