Mwakilishi
wa Wananchi wa Shehia ya Kilimani Kidoti Mkoa wa Kaskazini Unguja
akiwasilisha changamoto zinazowakabili wananachi wa Kijiji hicho mbele
ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo
pichani aliyefika kuitika wito waliomuagiza.
Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Kilimani Kidoti wakisikiliza nasaha za Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif baada ya kumueleza changamoto wanazopambana nazo kijijini pao.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwaahidi Wananchi wa
Kijiji cha Kilimani Kidoti kwamba Serikali Kuu itazingatia changamoto
zinazowakabili na kuzifanyia kazi inayostahiki.
MAKAMU
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameahidi kufutilia na
hatimae Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutafuta mbinu za kutanzua
changamoto zinazowakabili Wananchi wa Shehia ya Kilimani Kidoti Jimbo la
Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema
changamoto hizo zikiwemo fidia ya nyumba, mazao, Madrasa pamoja na
uvamizi wa eneo la Ardhi zitapatiwa ufumbuzi bila ya kuleta hitilafu kwa
upande wowote uliohusika na changamoto hizo.
Balozi
Seif Ali Iddi alitoa ahadi hiyo wakati akizungumza na Wananchi wa
Shehia ya Kilimani Kidoti mara baada ya kupokea kero zinazowakabili
ambazo nyengine zina muda mrefu sasa bila ya kupatiwa ufumbuzi Mkutano
uliofanyika katika Skuli ya Maandalizi ya Kilimani Kidoto Jimbo la
Nungwi.
Alisema
Mwananchi wote wa Taifa hili wanahitaji kupata maendeleo katika maeneo
wanayoishi kwa vile maendeleo hayo hayana itikadi, kabila, rangi, dini
wana sehemu wanayotoka.
Balozi
Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalielewa tatizo la
Wananchi hao kuhusu fidia za mali na mazao yao kufuatia kupita kwa Bomba
ya huduma za maji safi na salama katika Kijiji chao.
Alisema
juhudi zitachukuliwa na Serikali Kuu kupitia Wizara ya Fedha kulipa
fidia ya mali na mazao ya Wananchi hao kadri hali itakavyoruhusu kwa
lengo la kuwaondoshea usumbufu Wana Kijiji hao hasa wale waliobomolewa
nyumba zao.
Akizungumzia
suala la Maskani ya CCM ya Kijiji hicho iliyohodhiwa na upande wa
Upinzani Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri
Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi aliwanasihi Wana CCM wa Kijiji hicho
kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa Jengo jengine.
Alisema
yeye binafsi atakuwa tayari kusaidia nguvu za uwezeshaji wa Vifaa kwa
ajili ya ujenzi huo hatua ambayo itaondosha fitna, majungu na mgongano
unaoweza kuleta athari hapo baadaye baina yao na wale wa Upinzani
walioamuwa kuihodhi maskani yao.
Naye
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi
aliwataka Wananchi wa Kijiji hicho kuwa na subra huku akitafuta nguvu za
ufadhili ili kuanza kuunga mkono ujenzi wa Madrasa ya Kijiji hicho.
Mama
Asha alisema hatua zitachukuliwa katika kutoa vifaa vitakavyoanzia
ujenzi huo ili kutekeleza ahadi iliyotolewa kwa Wana Kijiji hao
kusaidiwa nguvu za ujenzi huo.
Wakitoa
changamoto zinazowakabili baadhi ya Wawakilishi wa Wananchi hao
walilalamikia lugha za Ubabe zinazotolewa dhidi yao kutoka kwa baadhi
ya Viongozi wanaoteuliwa na Serikali.
Walisema
licha ya jitihada wanazoendelea kuchuku za kufuatilia changamoto
wanazopambana nazo katika ngazi mbali mbali kuanzia shehia hadi Mkoa
lakini bado wamekuwa wakipambana na lugha mbovu zisizostahiki kutolewa
na Viongozi hao.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
14/10/2015.
Post a Comment