Chama
cha Mapinduzi (CCM) kimelaani vikali kitendo cha Mgombea Urais wa
Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF) kujitangaza mshindi kinyume na
sheria ya Uchaguzi huku ikiishangaa Tume ya Uchaguzi Zanzibar-ZEC kwa
kukaa kimya dhidi ya kitendo hicho.
Akizungumza
na waandishi wa habari jioni hii, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,
Vuai Ali Vuai amesema kitendo cha Maalim Seif kujitangaza mshindi
kimekiuka sheria ya uchaguzi na kuhoji dhamira ya kiongozi huyo kufanya
hivyo.
“Ni
tukio la kushitusha sana na hatujui malengo ya kitendo hiki au anataka
kuitia nchi katika mtafaruku?” Alihoji Vuai na kuitaka ZEC itekeleze
majukumu yake kwa kuzingatia Katiba na Sheria.
Katika
mkutano huo, Vuai alieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya matukio
yaliyotawala uchaguzi huo ambayo aliyaeleza kuwa yalilenga kukihujumu
chama hicho ili kuharibu ushindi wa wagombea wake.
“Huko
Pemba katika jimbo la uchaguzi la Chonga wakala wa CUF alikamatwa na
karatasi za kupigia kura akishirikiana na afisa wa Tume” alieleza Vuai
na kuhoji ni kura ngapi zimepita bila ya kugunduliwa.
Aidha,
chama hicho kilieleza kitendo cha wakala wake wote katika Wilaya za
Magharibi ‘A’ & ‘B’ kutopewa vitambulisho kilikuwa na lengo la
kuharibu ushindi wa chama hicho kwa kuwa ZEC iliruhusu uchaguzi
kuendelea kwa muda mrefu bila ya kuwepo mawakala wake.
“Tulikwenda
Tume tarehe 24 Oktoba, 2015 tukahakikishiwa na kwa kuviona vitambulisho
vya mawakala wa vyama vyote, lakini siku iliyofuata tulipokwenda
kuvichukua vyetu tukaambiwa havionekani” alifafanua Vuai na kuhoji
kilichotokea baina ya upigaji wa kura ulipoanza saa moja hadi wakala wa
kwanza kupata kitambulisho baada ya saa karibu nne ambapo sehemu
nyingine wakala wao walifika saa saba hawajapata vitambulisho.
Alipoulizwa
kuwa malalamiko hayo yanamaanisha chama chake hakina imani na ZEC,
Naibu Katibu Mkuu huyo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa chama chake
bado kinaiamini Tume hiyo lakini inaikumbusha wajibu wake.
“CCM
ni chama kikubwa,tujiulize kama tukio hili lingewakuta wenzetu wa CUF
ingekuwaje. Kwa nini vitambulisho vyetu vipotee katika eneo lenye wapiga
kura wengi zaidi kuliko sehemu nyingie yeyote Zanzibar”alifafanua Vuai
na kuongeza kuwa wajibu wa kutii sheria ni wa kila mtu na kila chombo
hivyo isingekuwa busara kwa CCM kukaa kimya kwa yaliyotokea.
Wakati
huo huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Shamsi Vuai Nahodha amesema
kitendo cha Maalim Seif kutangaza matokeo ni njama za kuishinikiza Tume
ya Uchaguzi kufuata matakwa yao.
“Kitendo
cha Maalim kujitangazia ushindi ni njama za kuishinikiza ZEC ifanye
kile inachokitaka. Tungeelewa kama wajumbe wa ZEC kutoka chama cha CUF
wangekuwa wamejizulu”alieleza Shamsi wakati wa kujibu maswali kutoka kwa
waandishi wa habari.
Akijibu
swali kuhusu lawama kuwa serikali imeleta askari wengi vituoni, Shamsi
ambaye ni Waziri Kiongozi mstaafu na pia amewahi kushika nafasi ya
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alisema vyombo hivyo
vinafanyakazi wakati wote si wakati wa uchaguzi tu na viko kuhakikisha
ulinzi wa wananchi na mali zao.
Leo
asubuhi Maalim Seif Sharif Hamad alitangaza ‘matokeo’ ya uchaguzi mkuu
kinyume na sheria ambapo alijitangaza mshindi wa nafasi ya urais.
“Hoja
ya msingi hapa yupo mtu amefanyakazi kinyume na Katiba na
Sheria.Tumekuja kukumbushia wajibu wa kufuata Katiba na Sheria, tunataka
muielimishe jamii kuwa kitendo cha Maalim kujitangazia ushindi ni cha
uvunjifu wa Katiba na Sheria” Alieleza Mheshimiwa Haji Omar Heri.
Post a Comment