Ili kupata hati ya ushindi Mbunge Mteule wa jimbo la Serengeti Mkoa wa Mara Marwa Ryoba (Chadema)alilazimika kumkaba Msimamizi wa Uchaguzi jimbo hilo,baada ya kutomkabidhi hati yake ya ushindi.
Tukio
hilo lililovuta umati mkubwa wa watu wakishinikiza msimamizi huyo atoe
hati lililazimu polisi kupiga mabomu ya machozi ili kutawanya watu ambao
walikuwa wamezunguka uzio wa ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji.
Kabla
ya kutokea kwa tukio hilo Ryoba alilazimika kupiga kelele akiwataka
wananchi waliokuwa wamezingira ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa
halmasahuri hiyo wakisubiri mbunge wao akabidhiwe hati ,huku akidai kuwa
kuna mkakati wa kumchakachua unaoongozwa na msimamizi wa uchaguzi Naomi
Nnko.
“Toka
saa 10 jioni mara baada ya kunitangaza msimamizi anapiga piga chenga
kunipa hati ya ushindi,amekuwa na maneno mengi …mara njoo kesho,nawajua
hawa toka mapema amekuwa na mjadala na dk Stephen Kebwe,nimelazimika
kuomba wananchi kwa kuwa wao ndiyo wamenichagua,ni haki yao toka saa
kumi hadi saa moja anazungusha tu na watu hawatoki bila mimi kupata
hati”alisema.
Hata
hivyo kutokana na kushindwa kutoa hati mapema hali ilichafuka na
wananchi wakaanza kurushia mawe askari polisi wakalazimika kupiga
mabomu ya machozi ,hata hivyo kundi lingine lilianza kupiga mawe ofisi
ya Takukuru na wengine ofisi ya idara ya fedha na kupasua
kioo,msimamizi huyo alilazimika kuchapa hati na kumkabidhi mbunge.
Akizungumzia tukio hilo Msimamizi wa Uchaguzi huku akilalamika alisema alikabwa na kusukwa sukwa na mbunge huyo na kuwa yeye hakuna na sababu ya kumnyima hati bali hakuwa na funguo za ofisi.
“Jamani
hivi kweli mtatuongoza kwa staili hii tutafika,mimi nimekabwa na mbunge
nikaburuzwa kuwa nitoe hati,nimemweleza sina funguo lakini
analazimisha,lazima tujenge misingi mizuri ya kuheshimiana kwa kuwa
tutafanya kazi pamoja,”alisema.
Hata
hivyo wakati wa makabidhiano ya hati msimamizi huyo hakutaka kupigwa
picha na mbunge huyo kwa madai kuwa yeye haitaji picha,”sihitaji picha mimi”alisema huku anamkabidhi akiwa amekaa kwenye kiti.
Hata
hivyo baadhi ya watendaji wa serikali na wananchi walisema kuwa chanzo
cha fujo huwa ni wasimamizi wenye maslahi binafsi na vyama ama wagombea
na si polisi,kwa tukio hilo wananchi walikuwa tayari kwa lolote kwa
kuwa walikubali kunyeshewa na mvua ili kuhakikisha mbunge wao anapata
haki,na kulazimisha matumizi ya nguvu bila sababu za msingi.
Mwenyekiti
wa Chadema wilaya Sang’uda Manawa alisema kuwa wasimamizi ni chanzo cha
migogoro katika chaguzi hasa wanapoingiza mapenzi yao badala ya
kuzingatia sheria,kwa kuwa kundi hilo lilikuwa tayari kwa lolote na
huenda kungetokea tukio baya ili kulinda haki yao isiporwe.
Kuhusu
matukio mengine ya uvunjifu wa amani jimboni polisi walisema hali ni
shwari na kuwa walijitahidi kudhibiti vikundi vya watu waliokuwa
wamejipanga kuvuruga uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Wakati
huo huo wafanyabiashara waliokuwa wamefunga kazi zao kwa siku mbili
wakihofia matukio mabaya kabla ya kutangazwa kwa matokeo wameendelea na
kazi kama kawaida huku mji ukiwa shwari.
Post a Comment