Zanzibar:
Mgombea wa Urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amemuomba Rais
Jakaya Kikwete na Rais Ali Mohamed Shein kubeba dhamana ya uongozi
katika siku hizi chache zilizobaki za uongozi wao kwa kusimamia katiba
na sheria za nchi.
MgombeaUrais
wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Chama hicho Mtendeni
Zanzibar. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed
Mazrui. Picha: OMKR
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake Mtendeni Maalim Seif amesema
marais hao wawili kuheshimu maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe
25 Oktoba na kuwataka washirikiane nae katika kuinusuru Zanzibar.
“Nawaomba
sana Rais Kikwete na Rais Shein kukwepa matumizi ya nguvu na badala
yake tushirikiane kutunza amani na haki za wananchi. Mimi niko tayari
kushirikiana nao kama ambavyo nimekuwa nikifanya mara zote. Tushirikiane
kuiepushia Zanzibar na Tanzania fedheha ya kimataifa”. Alisema Maalim
Seif.
Akizungumzia
kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi iwapo ni halali au sio halali Maalim
Seif amesema lile lilikuwa ni tamko binafsi la Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha ambapo Chama Cha Wananchi
(CUF) kimetiwa nguvu na tamko la Makamishna wawili wa Tume
waliothibitisha kwamba tamko lile ni lake binafsi.
“Ni
kwamba hakukuwa na kikao cha Tume kilichokaa kuamua yaliyosemwa na
Jecha, na kwamba hakuna misingi ya kikatiba na kisheria ya tamko lile”
alisema Maalim Seif na kuongeza kwamba.
“Jana
jopo la wanasheria wa CUF lilikutana kuangalia kwa kina kama kuna
misingi ya kikatiba na kisheria ya tamko lile binafsi la Jecha Salim
Jecha, na limetoa hoja za msingi zifuatazo kwa kuanzia muundo wa Tume
ambapo Kifungu 119(1) kinaanzisha Tume ya Uchaguzi yenye wajumbe saba
(7) akiwemo Mwenyekiti wao.
Alisema
(1) Kifungu 119 (10) kinatamka kuwa: “Kiwango cha mikutano ya Tume ya
Uchaguzi ni Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wane na kila
uamuzi wa Tume ni lazima uungwe mkono na Wajumbe walio wengi”.
Aidha
alisema (1) Kwa sababu Tume haikukaa kwa pamoja ikiwa na Mwenyekiti au
Makamu Mwenyekiti na angalau wajumbe wengine wanne, na kwa sababu
maamuzi yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume yalikuwa ni yake peke yake,
maamuzi hayo kikatiba ni batili na hayana nguvu zozote.
Maalim
Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF alisema waangalizi wote wa uchaguzi
ikiwa ni pamoja na SADC, AU, Commonwealth Observer Team, European Union
Election Observation Team, Waangalizi kutoka Uingereza na Marekani, na
TEMCO, wote walisema mbali na dosari ndogo ndogo uchaguzi ulikuwa huru,
wa haki na amani.
Aidha
aliwaambia waandishi wa habari kwamba Mwenyekiti wa ZEC mwenyewe naye
pia alisema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki ambapo Mwenyekiti huyo huyo
alisimamia kazi ya uhakikiwa matokeo na kutia saini fomu za matokeo
yaliyohakikiwa na kuthibitishwa za majimbo 31 ya Unguja na kuyatangaza
matokeo hayo kabla.
“Kwa
nini ghafla ilipofika siku ya tatu ambayo ni jana aligeuka na kukataa
kuendelea na uhakiki na badala yake kudai eti kulikuwa na mambo kadhaa
ya kufanya uchaguzi huo usiwe huru na wa haki? Tena dosari zenyewe za
tamko lake eti ni pamoja na wajumbe wake kuvua mashati na kutaka
kupigana” alisema Maalim.
Akizungumzia
suala la baraza la Wawakilishi jipya Maalim Seif alisema Kifungu 92(1)
cha Katiba ya Zanzibar kinaeleza kwamba maisha ya Baraza la Wawakilishi
ni miaka mitano tokea lilipoitishwa mkutano wake wa mwanzo hivyo Kifungu
90(1) kinaeleza kwamba mkutano wa mwanzo wa Baraza la Wawakilishi
utafanyika si zaidi ya siku 90 tokea Baraza lilipovunjwa kwa ajili ya
kuitishwa uchaguzi.
Kuna
masuali kadhaa ya kujiuliza alisema Maalim Seif ikiwemo ni “Rais yupi
ataitisha Baraza?, Wawakilishi wapi wataitwa (wakati hawapo)?, Yote haya
yanaleta mgogogro wa kikatiba ambao umesababishwa na mtu mmoja
anayeitwa Jecha Salim Jecha kwa sababu tu ya kufuata maelekezo ya chama
chake cha CCM”. Alihoji Maalim Seif huku akionekana kuongea kwa
kujiamini.
Hata
hivyo alisema kuna suali la muundo wa mpito ambapo kama uchaguzi
utarejewa, kama anavyotaka Mwenyekiti wa Tume, jambo ambalo alisema
halikubaliki kwa sababu ya kukosa misingi ya kikatiba na kisheria, ina
maana kuwa serikali itakuwa haipo.
Akitoa
sababu za kutokuwepo Maalim Seif alisema kwanza muda wa Urais ni miaka
mitano kuanzia tarehe aliyochaguliwa kwa mujibu wa kifungu 28(2) cha
Katiba, Ingekuwa tamko la Jecha Salim Jecha ni halali, basi maana yake
hakuna Rais anayefuata kwa sababu ya kufutwa kwa uchaguzi, hivyo
hakutakuwa na kiapo cha kumuapisha rais mpya. Kwa msingi huo, msharti ya
kifungu cha 28(1)(a) hayana nafasi katika mtafaruku huu uliosababishwa
na mtu mmoja.
“Hiyo
maana yake, kipindi hicho sasa kitakuwa tete na haijulikani kikatiba ni
nani ataongoza nchi? Tunasema hivyo kwa sababu vifungu vya Katiba 33(1)
na (2) havitumiki hapa kwa suala la kuwa wazi kwa kiti cha Urais na
kukaimiwa kwa nafasi hiyo”. Aliongeza.
Alisema
hiyo ni kwa sababu nafasi ya Urais haipo kwa sababu itakuwa imemaliza
muda wake ifikapo tarehe 2 Novemba, 2015, siku ambayo Urais wa Dk. Ali
Mohamed Shein unakamilisha miaka mitano kamili.
Halikadhalika
Maalim Seif alitaka kujua jee katika suala hilo suluhisho ni nini?
“Kutokana na hoja tulizozieleza hapo juu, ni wazi kwamba tamko la Jecha
Salim Jecha ni lake binafsi na kama tulivyotangulia kusema, halina
misingi ya kikatiba na kisheria. Kwenye taarifa yake alisema kuwa “...
kwa uwezo nilionao …”. Masuala ya kujiuliza ni uwezo upi? Chini ya
kifungu kipi cha Katiba au Sheria ya Uchaguzi?” alihoji.
Katika
kutilia nguvu hoja yake hiyo ya kisheria Maalim Seif alisema kwa
kifupi, ni kwamba Mwenyekiti wa ZEC uwezo huo hana kikatiba na kisheria
na kwa msingi huo, maamuzi yake hayo ni batili.
Kufuatilia
masuali hayo ambayo majibu yake yapo kisheria Maalim Seif alisema CUF
inasisitiza kile kinachodaiwa na waangalizi wote wa uchaguzi waliotoa
taarifa zao kwamba uamuzi wa Mwenyekiti wa ZEC ni uamuzi wake binafsi
pekee na haukuwa uamuzi wa Tume, kwani hakukuwa na kikao chochote cha
Tume kilichokaa kufikia uamuzi huo.
Alisema
uamuzi huo uwekwe upande na Jecha Salim Jecha amepoteza sifa ya
uadilifu ambayo ni msingi mkuu wa kazi ya Tume ya Uchaguzi katika
kusimamia maamuzi ya Wazanzibari ambao kikatiba (kwa mujibu wa kifungu
cha 9(2) (a) ndiyo wenye mamlaka ya kuwaweka madarakani viongozi wa
Serikali.
“Hivyo,
anapaswa awajibike kwa hatua yake ya kuiingiza nchi katika mgogoro
pasina sababu yoyote na ajiuzulu” alisema Maalim Seif huku akionekana na
furaha katika mkutano huo wa waandishi wa habari.
Aidha
alishauri Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar waendelee na kazi ya
kukamilisha uhakiki na majumuisho ya matokeo ya uchaguzi kwa majimbo 14
yaliyobaki na kisha kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa Rais wa Zazibar.
Alisema
baada ya ukamilishaji huo alisema mshindi wa nafasi ya Urais wa
Zanzibar aapishwe, Viongozi wa CUF na CCM washirikiane kuunda Serikali
mpya ya Umoja wa Kitaifa itakayoiongoza Zanzibar katika miaka mitano
ijayo.
“Kwa
maana hiyo, kitumike kifungu 42(6) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoeleza
kwamba kama kuna matatizo yoyote katika vituo vya kupigia kura a na
matokeo hayawezi kutolewa ndani ya siku tatu; basi Tume iendelee
kuhesabu na kuhakiki kura na kutangaza matokeo ndani ya siku tatu
nyengine na shughuli za kiserikali ziweze kuendelea” aliongeza.
Katika
hatua nyengine Malaim Seif alirejea tena kauli yake ya kuhimiza Amani
na kuwataka wafuasi wake na wananchama wa CUF na Wazanzibari wote kwa
ujumla kuendelea kuwa watulivu na kutunza amani ya nchi yetu huku
wakitambua kwamba tutayasimamia maamuzi yao waliyoyafanya tarehe 25
Oktoba, 2015.
Baadhi
ya wafuasi wa CUF wakiwa wamekusanyika nje ya ofisi za CUF Mtendeni
kusikiliza kauli za viongozi wao kuhusu maamuzi watakayochukua baada ya
kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi
Mgombea
Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya hoteli ya Bwawani
kabla ya kutolewa taarifa ya kufutwa kwa uchaguzi
Chanzo: zanzibariyetu.wordpress.com
Post a Comment