Polisi mkoani Mwanza jana walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa Chadema walioingia mitaani kushangilia wakiamini wagombea wao wanaongoza katika matokeo ya awali.
Tukio
hilo lilitokea kwenye kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi
Mlimani, eneo la Butimba, Ghana na Shule ya Msingi Buzuluga kwenye
majimbo ya Nyamagana na Ilemela.
Taarifa
toka jijini Mwanza zinasema kundi la watu waliokuwa vituoni wakisubiri
kubandikwa kwa matokeo hayo, lililipuka kwa shangwe, nderemo na
shamrashamra baada ya matokeo hayo kubandikwa na wasimamizi wa uchaguzi
wakiamini wagombea wao wanaongoza.
Baafa ya hali hiyo, polisi waliingilia kati na kufyatua mabomu ya machozi kutawanya wafuasi hao.
Katika
uchaguzi wa mwaka huu, mgombea ubunge wa Chadema na mbunge anayemaliza
muda wake katika jimbo la Nyamagana, Ezekiel Wenje anachuana vikali na
aliyekuwa Meya wa jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula wa CCM.
Katika
jimbo la Ilemela, mbunge anayemaliza muda wake, Highness Kiwia wa
Chadema anatetea nafasi yake kwa kupambana na mgombea wa CCM, Anjela
Mabula.
Uchaguzi
wa urais, ubunge na udiwani umefanyika jana Oktoba 25, mwaka huu ambapo
takribani Watanzania milioni 22.7 wamejiandikisha kwenye daftari la
kudumu kwa upande wa Tanzania Bara huku kwa upande wa Zanzibar zaidi ya
wapigakura laki tano wamejiandikisha.
Post a Comment