THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amepokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Waziri wa
Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Abdallah Omari Kigoda ambaye aliaga
dunia jana, Jumatatu, Oktoba 12, 2015 katika Hospitali ya Apollo mjini
New Delhi, India, ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu tokea Septemba
19, mwaka huu. Alikuwa na umri wa miaka 62.
Katika
salamu za rambirambi ambazo amemtumia Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo
Peter Kayanza Pinda, Rais Kikwete amesema: “Kwa hakika, nimeshtushwa na
kuhuzunishwa mno na taarifa za kifo cha Waziri Kigoda ambacho
nimetaarifiwa kuwa kimetokea India ambako alikuwa anapata matibabu tokea
mwezi uliopita.”
Ameongeza
Rais Kikwete katika salamu zake hizo za rambirambi: “Kama unavyojua,
namfahamu vizuri Mheshimiwa Kigoda. Alikuwa Waziri wangu. Nimefanya kazi
naye kwa karibu na kwa miaka mingi ndani ya Serikali yetu. Alikuwa
mtumishi hodari, mtumishi mwaminifu na mwadilifu kwa wananchi wa
Tanzania, na hasa wananchi wa Jimbo la Handeni, ambao aliwawakilisha kwa
miaka mingi akiwa Mbunge wao. Tutakosa utumishi wake mahiri sana.”
“Nakutumia
wewe Mheshimiwa Pinda, Waziri Mkuu wa nchi yetu salamu za rambirambi za
dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo cha Mheshimiwa Kigoda. Aidha,
kupitia kwako namtumia rambirambi nyingi Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anna Semamba Makinda na Wabunge wote
kwa kuondokewa na mwenzao.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Nakuomba pia unifikishe salamu zangu za rambirambi kwa
wananchi wa Jimbo na Wilaya ya Handeni ambao wamepoteza Mbunge wao
aliyewatumikia kwa ustadi mkubwa kwa miaka mingi. Aliwawakilisha vizuri
na kujali sana maslahi yao. “
Amesisitiza
Rais Kikwete: “Kupitia kwako, Waziri Mkuu pia naitumia familia, ndugu,
jamaa na marafiki wa Mheshimiwa Kigoda kwa kuondokewa na mhimili wa
familia na rafiki yao mpenzi. Yajulishe makundi yote hayo kuwa niko nao
katika msiba huu mkubwa, uchungu wao ni uchungu wangu na majonzi yao ni
majonzi yangu. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu ya
uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi. Pia naungana nao
kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya Dkt. Abdallah Omari
Kigoda”. Amen.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
13 Oktoba, 2015
Post a Comment