Bendera na ramani ya Tanzania |
JUMAPILI ya
Oktoba 25, 2015, Tanzania inafanya Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge
pamoja na kumpata Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Uchaguzi
ni nini? Zipo tafsiri mbalimbali lakini mojawapo na iliyo wazi ni
kwamba, hii ni njia ya kidemokrasia inayotumiwa na watu katika kuchagua
viongozi wa kuwaongoza kwa kipindi fulani kwa mujibu wa Katiba au
utaratibu waliojiwekea wenyewe.
Huu
ni Uchaguzi Mkuu wa Tano kufanyika tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza
tena mwaka 1992, lakini ni wa 11 tangu Tanganyika na Zanzibar
zilipoungana mwaka 1964.
Uchaguzi
wa mwaka huu una umuhimu wa kipekee kwa sababu kadha wa kadha, mojawapo
ikiwa umri wa miaka 23 tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza.
Huu
ni umri mkubwa, na kwa hakika vijana wengi waliojitokeza kujiandikisha
safari hii ni wenye umri wa kati ya miaka 18-35, ikimaanisha kwamba
wengi wao walizaliwa kuanzia mwaka 1992.
Hawa
wanatengeneza asilimia 57 ya wapigakura wote. Umuhimu mwingine ni
kwamba, kulinganisha na uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995,
safari hii demokrasia imekua na kupanuka kiasi cha kushuhudia wapigakura
22.75 milioni, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini tangu
tupate Uhuru.
Kwa
upande mwingine, uhuru wa habari umepanuka ukiwamo ukuaji wa sekta ya
habari na mawasiliano, hususan mitandao ya kijamii. Haya yote yanatokea
kutokana na kuwapo kwa amani na utulivu, sifa ambazo zimeendelea
kuitambulisha vyema Tanzania hata katika jumuiya za kimataifa.
Uchaguzi
Mkuu ni gharama kubwa kifedha, rasilimali watu na muda, na kama mambo
yatakwenda mrama maana yake nchi itakuwa imeingia hasara kwa kupoteza
fedha, lakini pia itaingia kwenye machafuko ambayo yatatowesha amani
iliyodumu kwa miaka mingi.
Madhara
ya machafuko au vita – kama tulivyoshuhudia kwa majirani zetu Rwanda na
Kenya ni vifo, ulemavu wa kudumu, kutengana na familia, ukimbizi na
kuvurugika kwa uchumi, jamii na siasa kwa ujumla. Kwa miaka yote tangu
Uhuru, licha ya uchanga na umaskini kama taifa, Watanzania hatujazoea
maisha ya vurugu na machafuko na ndiyo maana tuna wajibu wa kuhakikisha
uchaguzi huu unapita salama.
Wajibu
wa kulinda amani ya nchi yetu ni wa kila Mtanzania bila kujali rangi,
dini, kabila ama nafasi yake katika jamii. Tunaposema hivyo tunamaanisha
kwamba, vyombo vya dola vinapaswa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa
sheria na kuhakikisha Watanzania wanapiga kura kwa amani kuchagua
viongozi wao kwa utaratibu waliojiwekea.
Kimsingi,
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndio wasimamizi wa chaguzi zote, hivyo
wana dhamana kubwa kuhakikisha kila aliyejiandikisha na kujitokeza siku
hiyo anatumia haki yake ya kikatiba kupiga kura bila kubughudhiwa. Ili
kuondoa utata huo, NEC pia inapaswa kuhakikisha kunakuwa na uwazi
kuanzia hatua ya kupiga kura mpaka wakati wa kutangaza matokeo, ambayo
pia yanatakiwa kutolewa kwa wakati ili kuondoa mashaka miongoni mwa
wagombea na wananchi kwa ujumla.
Wanasiasa,
hususan wagombea ama wapambe wao, wanapaswa kutoa kauli za kuhamasisha
amani na utulivu kwa siku hizi chache zilizosalia kuelekea uchaguzi
mkuu, siku ya uchaguzi na baada ya kutangazwa kwa matokeo.
Wanasiasa
wanaaminika kwa wananchi, kwa hiyo kauli yoyote watakayoitoa ama
inaweza kujenga au kubomoa amani iliyopo, hivyo kuondoa utulivu na
kuisambaratisha Tanzania ya sasa iliyotukuka ulimwenguni kote kama
kisiwa cha amani na utulivu.
Vyombo
vya habari navyo vina wajibu mkubwa zaidi kuhakikisha uchaguzi
unafanyika kwa usalama na amani na hata baada ya matokeo kutangazwa
viendelee kudumisha amani hiyo. Hilo litawezekana tu iwapo vyombo vya
habari vitaandika au kutangaza habari kwa kufuata sheria za nchi, miiko
na maadili ya taaluma na fani ya uandishi wa habari ikiwa ni pamoja na
kutoegemea upande wowote, kuepuka lugha za uchochezi na ushabiki wa
kisiasa, kabla na wakati wa kutangaza matokeo.
Kutokana
na umuhimu huo, sisi wamiliki wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania
(Bloggers) tumejadiliana na kukubaliana kwa pamoja kuhusu hatma na
mustakabali wa taifa letu kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa
wakati na baada ya uchaguzi huu wa kidemokrasia na kwa kauli moja
tumetoa msimamo wetu kuhusu amani ya nchi hii.
Kwa
ujumla, hakuna anayeweza kujisifu kuwa ana uhalali zaidi wa taifa hili
kuliko mwingine, taifa hili ni letu sote, hivyo wajibu wa kulinda na
kudumisha amani na usalama wa nchi ni wa kila mmoja.
Tunaomba
Watanzania wote wenye sifa wajitokeze kupiga kura kwa amani na utulivu,
wasubiri matokeo kwa amani na utulivu, wapokee matokeo kwa amani na
utulivu, maisha yaendelee kwa amani na utulivu, tusonge mbele kwa amani
na utulivu huku tukijua kwamba kuna maisha baada ya uchaguzi, na hilo
ndilo muhimu zaidi.
MUNGU IBARIKI TANZANIA!
Post a Comment