Baada ya upepo wa Uchaguzi Mkuu kuanza kutulia, baadhi ya makada wa CCM wameanza kutuhumiana kuwa unafiki na hujuma zilizofanywa na baadhi ya wanancha wa chama hicho zimesababisha kishindwe kufanya vizuri katika baadhi ya maeneo kwa ngazi za udiwani na ubunge.
Baadhi
ya makada hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakieleza kuwa CCM ina
‘wanafiki’ wengi ambao wanaangalia zaidi masilahi yao kuliko chama.
Hata
Rais mteule, Dk John Magufuli amekuwa akizungumzia suala hilo tangu
kipindi cha kampeni, akilalamika kuwa kuna watu waliokuwa naye mchana
lakini usiku wanahamia Ukawa.
Dk
Magufuli alipigilia msumari suala hilo alipozungumza na wafuasi
waliojitokeza kumpokea katika ofisi ndogo za CCM, Lumumba baada ya
kupatiwa cheti cha ushindi wa urais na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC),
akisema kuna haja ya kukijenga upya chama hicho kwa kuwaondoa wanafiki
wote.
Dk
Magufuli alimweleza mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete huku
akimuomba radhi kwa maneno aliyoyazungumza kuwa akiona mnafiki amfukuze
mara moja kwa kuwa hakuna sababu ya kuwa na makada wengi ambao ni
wanafiki, ni bora kubaki na wachache waaminifu.
“Nisiposema
nitakuwa mnafiki, msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Watubu wajirekebishe.
Ni heri mara kumi kuwa na mpinzani kutoka nje kuliko ndani ya chama.
Mipango yenu mtaipanga mchana usiku wataitoa nje, ni afadhali uwe na
mchawi atakuroga ufe kuliko mtu mnafiki,” alisema Dk Magufuli.
Tuhuma
za unafiki zimeendelea kutawala ndani ya chama hicho, aliyekuwa mgombea
ubunge wa CCM Jimbo la Moshi Mjini, Davis Mosha juzi alitangaza
kuachana na siasa akidai kuwa chama hicho kimejaa wanafiki waliochangia
kuanguka kwake.
Mosha,
ambaye alisema ataendelea na biashara zake badala ya kufanya siasa,
alisema kushindwa kwake kulisababishwa na viongozi wa CCM kuanzia
Serikali za Mitaa, kata, wilaya hadi mkoa ambao alidai kuwa waliweka
mbele masilahi yao binafsi.
“Viongozi
wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro ni ndumilakuwili na nia yao si ushindi kwa
chama, bali wapo kimasilahi zaidi na hawana nia njema, ndio maana chama
kinashindwa,” alisema Mosha alipokuwa akiwashukuru wakazi wa Moshi Mjini baada ya kumalizika kwa uchaguzi.
Mfululizo
wa tuhuma za hujuma umeendelea katika maeneo mbalimbali nchini, huku
baadhi ya wanachama wa chama hicho katika Jimbo la Iringa Mjini,
wakimtuhumu Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Iringa, Jesca Msambatavangu
na viongozi wengine kwa kukihujumu chama hicho.
Wanachama
hao, walishinikiza Msambatavangu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Iringa
Mjini (UVCCM), Kaunda Mwaipyana na Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Mkwawa,
Salum Keita waachie ngazi au wachukuliwe hatua na chama kwa kusababisha
kupoteza jimbo na kata 14.
Hata
hivyo, Msambatavangu alikana tuhuma hizo na kuanisha kuwa kuna mambo
mengi yaliyofanyika kinyume na utaratibu na kusababisha jimbo hilo
kupotea kwa mara nyingine na kata 14.
Hali
hiyo imejitokeza pia wilayani Kilombero ambako baadhi ya wanachama wa
CCM wamewataka viongozi wao wa wilaya kung’atuka ndani ya siku 21
kuanzia jana, wakiwatuhumu kusababisha kupoteza majimbo mawili ya Mlimba
na Kilombero ambayo yamechukuliwa na Chadema.
Wanachama
hao 16 walioongozwa na Dismas Lyassa, walisema dalili za kuanguka kwa
chama hicho zilianza kuonekana mapema wakati wa uchaguzi wa Serikali za
Mitaa Desemba, mwaka jana, lakini hakuna hatua za dhati zilizochukuliwa.
Jambo
hilo limezidi kuwakera wengi kiasi cha kuwafanya wanachama wasiopungua
400 wa UVCCM Jimbo la Babati Mjini mkoani Manyara, kufanya maandamano
juzi hadi ofisi ya CCM mkoa wakiwatuhumu baadhi ya viongozi wa wilaya
kuhujumu uchaguzi na kusababisha jimbo hilo kuchukuliwa na Chadema.
Vijana
hao wakiwa na mabango yaliyokuwa na maandishi yaliyokuwa yakiwatuhumu
viongozi wanane wa juu wa chama hicho, waliandamana na kupokelewa na
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Lucas Ole Mukus.
Miongoni mwa waandamanaji hao, Steven Kairo alisema madai hayo yakithibitishwa, watuhumiwa wote wafukuzwe uanachama.
Alisema kama viongozi hawatayafanyia kazi madai yao, wao watakuwa wa kwanza kurudisha kadi.
“Tumehangaika
kuusaka ushindi wa CCM Babati Mjini, lakini ndumilakuwili
wakatuangusha, tunaomba mbariki ombi letu la kuwawajibisha viongozi hao,
watupishe, hata sisi tunaweza kuongoza,” alisema Kairo.
Post a Comment