RAIS
Mteule wa awamu ya tano katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John
Pombe Magufuli, ameshauriwa kuwa makini katika uundaji wa Baraza lake
la Mawaziri kwa kuepuka masuala ya kujuana au kuteua kwa shinikizo la
baadhi ya wanasiasa wenye masilahi binafsi.
Akizungumza na m,wandishi wetu
jana jijini Dar es Salaam, Mhadhiri mstaafu wa masuala ya Uongozi
katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro Dkt. Alfred Chimage, alisema
tatizo kubwa la viongozi wa Tanzania ni kutokuwa na uwezo wa kutambua
watu wanaofaa, wanaopaswa kuwateua ili kuwasaidia kuongoza nchi.
Aliongeza
kwamba viongozi wengi waliofanikiwa ni wale wenye uwezo mkubwa wa
kupanga timu sahihi ya wasaidizi katika masuala ya uongozi.
Dkt. Chimage alisema Dkt.
Magufuli anaweza kuwa kiongozi mzuri lakini hofu iliyopo anaonekana
kuzungukwa na kundi kubwa la wanasiasa hususan wanaoamini kwamba wametoa
mchango mkubwa kwake kumfikisha hapo alipo; hivyo kutaka kupata fadhila
za nafasi za juu za uongozi kwa ajili ya ndugu zao wa karibu na hata
watoto wao.
"Inawezekana
Magufuli ni kiongozi mzuri, lakini ukiangalia anavyoonekana ni kama
tayari amemezwa na baadhi ya wanasiasa wanaojinasibu na kujiona kana
kwamba amefikia hatua hiyo kwa nguvu yao.
"Mbali
na hilo, ukiangalia mazingira ya siasa zinazomzunguka ni kama kwamba
kuna kundi la wanasiasa wakongwe ndani ya CCM linaloamini kwamba
litaendelea kumpa maelekezo kwa hatua mbalimbali ikiwemo ya kuteua
baraza la mawaziri.
"Akinaswa kwenye mtego huo atakuwa amefanya kosa kubwa la kwanza kwenye uongozi wake," alisema mtaalamu huyo na kuongeza;
"Kuna
wanasiasa wengi ambao unawaona moja kwa moja wanajisogeza kwa nguvu
sana kwa Magufuli si kwa kumsaidia kuongoza nchi peke yake, bali wana
malengo maalumu kuhakikisha wananufaika kwenye uongozi wake kwa ndugu,
jamaa na hata watoto wao kupewa madaraka ya juu".
Alisema
katika kipindi hiki, Dkt. Magufuli anapaswa kuwa makini zaidi ili
kuepusha Serikali yake kupoteza imani mbele ya Watanzania kwa kuendekeza
kile kinachofahamika kama siasa za kujuana na kubebana kama njia ya kulipa fadhila.
Alisema
Dkt. Magufuli anapaswa kutambua kwamba yeye ni rais wa Watanzania wote
na si rais wala rafiki ya familia au kundi fulani la watu, hivyo
anapaswa kuteua mawaziri na watendaji wengine kwa kigezo cha uwezo.
"Magufuli asipokuwa makini malalamiko ya kwanza ya wananchi yatakuja baada tu ya kutangaza Baraza lake la Mawaziri, kama litaonekana kubeba watu kwa misingi ya kujuana. Anachopaswa kufanya ni kuacha mamlaka husika zifanye proper vetting (Uhakiki wa kina) wa sifa za kila anayeona anafaa".
"Magufuli asipokuwa makini malalamiko ya kwanza ya wananchi yatakuja baada tu ya kutangaza Baraza lake la Mawaziri, kama litaonekana kubeba watu kwa misingi ya kujuana. Anachopaswa kufanya ni kuacha mamlaka husika zifanye proper vetting (Uhakiki wa kina) wa sifa za kila anayeona anafaa".
"Asiteue baraza kwa misingi ya huyu ni rafiki yangu au ni ndugu au mtoto wa mtu fulani, hapana atajiharibia kabisa," alisema.
Ameshauri
pia kuwa makini kuepuka watendaji wote ambao kwa njia moja ama nyingine
walihusishwa na kashfa mbalimbali kwenye serikali iliyopita.
"Wakati
wa kampeni Magufuli ameimba sana neno mabadiliko, mabadiliko haya
yasiwe ya kusema tu. Wananchi wanasubiri waone mabadiliko hayo kuanzia
timu ya watu atakaowateua kufanya nao kazi. Watu wanatarajia kuona
mawaziri safi wasio na 'makandokando'.
"Anapaswa
kuwa makini na kila mtu. Atumie ile falsafa ya mke wa Kaisari. Aachane
na wote waliosemwa vibaya kwenye serikali iliyopita hata kama
wanaonekana kuchapa kazi. Mifano ipo mingi, waliochafuka kwa Escrow, kwa
uozo wa bandari, ununuzi wa mabehewa mabovu. Ili aingie kama kiongozi
safi na mtu wa mabadiliko ya kweli azibe mapema mianya kama hii.
Watanzania watapata imani na atafanikiwa," alisema.
Alisisitiza
kwamba Magufuli anapaswa kuwa makini kuepuka mitego ya kindugu, urafiki
na kifamilia ambayo alisema imeonekana kuwa tatizo kubwa katika masuala
ya uongozi hapa nchini.
Alisema kigezo pekee cha mtu kuteuliwa kuwa waziri au kiongozi wa nafasi yoyote ile ni kuchapa kazi.
Post a Comment