Hatimaye mchuano wa uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) umechukua sura mpya baada ya vigogo
kadhaa kutemwa wakiwamo spika wa zamani, Samwel Sitta na aliyewahi kuwa
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Naibu Spika wa Bunge la 11, Job Ndugai, Naibu Mwanasheria Mkuu, Dk.
Tulia Ackson na Mbunge wa Afrika Mashariki, Abdullah Ali Mwinyi ambaye
ni mtoto wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ‘Mzee Ruksa’ ndiyo waliopenya
katika mchujo uliofanywa na Kamati Kuu ya CCM jana, huku vyanzo
mbalimbali vikitaja suala la umri na makundi kuwa ni miongoni mwa sababu
zilizowaponza waombaji wengine 20 waliojitosa katika mbio hizo. Makada
23 wa CCM ndiyo waliokuwa wakiwania uspika kumrtihi Anna Makinda
aliyetangaza kustaafu.
Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mbali na kushinda nafasi ya
urais iliyotwaliwa na Dk. John Magufuli, CCM pia ilifanya vizuri ubunge
baada ya kutwaa majimbo 186 na hivyo mgombea yeyote atakayepitishwa na
chama hicho kuwania uspika atakuwa na nafasi kubwa ya kushinda dhidi ya
wapinzani ambao kwa ujumla walitwaa majimbo 74.
Bunge la 11 linatarajiwa kuanza kesho na Rais Magufuli anatarajiwa kulizindua Ijumaa.
MCHUJO ULIVYOKUWA
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Katibu wa CCM wa
Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema Kamati
Kuu (CC) ya chama chao ilikuwa na kikao maalum chenye ajenda moja tu ya
kuwapitisha wagombea wa nafasi ya spika.
Aliwataja Ndugai, Dk. Tulia na Abdulla Mwinyi kuwa ndiyo waliopitishwa
kuwania nafasi hiyo na mchakato wa kumpata mgombea mmoja utaanza leo.
“Kamati Kuu imewateua wanachama wa CCM watatu ambao wanapelekwa katika
kamati ya wabunge wa CCM kesho (leo) kwenda kuchaguliwa mmoja ili awe
mgombea wa uspika wa bunge,”alisema Nape.
Nape alisema majina ya watatu hao yatawasilishwa kwenye kamati ya
wabunge wa CCM leo saa 4:00 asubuhi makao makuu ya chama hicho mjini
Dodoma na kupigiwa kura huku mmoja atakayeshinda kati yao ndiye
atakayepelekwa bungeni kuchuana na mgombea wa upinzani kuwania kiti
hicho.
Kuhusu nafasi ya Naibu Spika, Nape alisema ratiba iliyotolewa juzi na
chama hicho ilikosewa kwa bahati mbaya kwani nafasi hiyo itashughulikiwa
na kamati ya wabunge wenyewe wa CCM.
“Sasa kwa mujibu wa kanuni za Chama Cha Mapinduzi, suala la Naibu Spika
halishughulikiwi na kamati kuu bali na kamati ya wabunge wa CCM,”alisema
Katibu huyo.
Alifafanua kuwa kanuni za CCM, toleo la nne la mwaka 2011, ibara ya 57,
inasema mwanachama wa CCM anayetaka kugombea nafasi ya Naibu Spika wa
Bunge atajaza fomu maalum ya maombi na kuiwakilisha kwa katibu wa kamati
ya wabunge wote wa CCM katika muda ambao umewekwa.
“Ada ya fomu hiyo ni shilingi laki moja ambazo zitatolewa wakati
akirudisha fomu kwa katibu wa kamati. Kwa hiyo suala la Naibu Spika
kutoka CCM litamalizwa na kamati ya wabunge wa CCM,” alisema Nape.
Kadhalika, alisema kwa mujibu wa ratiba, wabunge wa CCM wanaotaka
kugombea nafasi hiyo watachukua fomu kuanzia leo (Novemba 16) na
kuzirudisha kesho kabla ya saa 10:00 jioni.
Aliongeza:”Uchaguzi utafanywa na wabunge wa CCM na unategemewa kufanyika
tarehe 17 (kesho) kumpata mgombea mmoja wa nafasi ya unaibu spika.
KILICHOWAPONZA
Vyanzo mbalimbali viliiambia Nipashe jana kuwa miongoni sababu
zilizowapa nafasi Ndugai, Mwinyi na Dk. Tulia ni kutokuwa na makundi,
ujuzi wa masuala ya sheria na pia umri.
Kadhalika, imeelezwa kuwa mbali na sababu hizo, vigezo vingine
vinavyodaiwa kuzingatiwa ijapokuwa havikutajwa wazi ni pamoja na jinsia
na pia umuhimu wa kuwa na sura ya muungano walau katika nafasi tatu za
wagombea.
Ndugai ana uzoefu wa kutosha kwani ndiye aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge
la 10, Abdullah ni kijana ambaye pia ana uzoefu na masuala ya Bunge
kwani hadi sasa ni Mbunge wa Afrika Mashariki na pia anatokea Zanzibar.
Kwa upande wa Dk. Tulia, yeye ni msomi kijana aliyezaliwa mwaka 1976 na
aliwahi kufanya vizuri wakati alipokuwa Mjumbe katika Bunge Maalum la
Katiba.
Chanzo kimoja kimeiambia Nipashe kuwa kwa kuzingatia mambo hayo na
mengine kadhaa yanayohusiana na sifa za kawaida walizokuwa nazo makada
wote waliojitosa kuwania uspika, huenda ndiyo maana Sitta na Nchimbi
wakawa miongoni mwa wale walioachwa katika orodha ya wagombea watatu wa
mwisho.
“Sitta ana uzoefu mkubwa kuhusiana na masuala ya Bunge. Ni wazi kwamba
umri wake wa takriban miaka 70 unaweza kuwa sababu mojawapo ya kukosa
nafasi hii kwani vinginevyo, ni wazi kwamba naye asingekosekana katika
orodha ya wagombea watatu wa mwisho,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe
kuhusiana na kuenguliwa kwa Sitta ambaye inaelezwa kuwa alizaliwa mwaka
1942, zaidi ya miaka 70 iliyopita.
Kadhalika, kuhusiana na kukatwa kwa Nchimbi, chanzo kingine kiliiambia
Nipashe kuwa waziri huyo wa zamani atakuwa ameponzwa na makundi ndani ya
chama, hasa kutokana na ukweli kuwa kwa muda mrefu iliaminika kuwa yeye
alikuwa katika kambi ya Edward Lowassa ambaye alienguliwa katika mbio
za urais ndani ya CCM kabla ya kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
Imeelezwa kuwa Nchimbi ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu (CC)
ni msomi na tena hana umri mkubwa kama Sitta, lakini kitendo chake cha
kukana maamuzi ya CC wakati alipoenguliwa Lowassa wakati wa mbio za
urais ndicho kilichomponza.
“Ni wazi kwamba Nchimbi ameponzwa na hisia za baadhi ya watu kwamba bado
yeye ni mtu wa karibu wa Lowassa… vinginevyo, ni wazi kwamba naye
asingekatwa kirahisi,” chanzo kiliiambia Nipashe.
Mbali na Sitta na Nchimbi, makada wengine wa CCM waliokuwa wakiwania
nafasi ya uspika ni pamoja na Gasbert Blandes na mawaziri wa zamani ,
Balozi Philip Marmo na Ritta Mlaki.
Akizungumza kwa njia ya simu, Sitta alisema bado hafahamu chochote juu ya kukatwa kwake.
“Sijaarifiwa. Siwezi kuzungumza chochote kwa kitu nisichokijua,
sijasikia na kawaida ninavyojua huwa tunaitwa na kuambiwa kasoro… hivyo
sijui sababu za kuondolewa kwangu. Inabidi tusubiri kwanza,” alisema
Sitta.
Miongoni mwa wagombea wa nafasi hiyo walioenguliwa, Banda Sonoko,
alisema yeye binafsi anapongeza mfumo uliotumika kupata majina hayo
matatu na hivyo anamuunga mkono yeyote atakeyepitishwa na Kamati ya
Wabunge wa CCM kuwa mgombea.
Mbunge mteule wa Chunya (CCM), Victor Mwambalaswa, alisema ni kanuni na
taratibu za chama zilizotumika kuwachuja na kuwapitisha wagombea watatu
na kwamba, uamuzi huo unadhihirisha kuwa ndani ya CCM hakuna kiongozi
mkubwa wala mdogo bali wanachama wote wana hadhi sawa.
Mbunge mteule wa Viti Maalum (CCM), Mkoa wa Mbeya, Dk. Mary Mwanjelwa,
alisema CCM inaongozwa kwa sheria na kanuni na hivyo maamuzi
yaliyotolewa na kikao cha kamati kuu yanapaswa kuheshimiwa, bila
kuangalia ni kina nani wameenguliwa.
Mbunge mteule wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy, alisema majina
yaliyopitishwa na kamati kuu yamezingatia jinsia, muungano na sifa za
kila mmoja.
“Hakuna mtu maarufu. Wote ni maarufu, mfano Mwinyi ni Mbunge wa Afrika
Mashariki, Dk. Tulia ni Naibu Mwanasheria Mkuu na Ndugai alikuwa Naibu
Spika katika Bunge la 10. Wote waliopitishwa wana sifa zinazostahili,”
alisema Kessy.
Mbunge mteule wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisema
mchakato huo utakuwa umetumia vigezo ambavyo yeye havifahamu lakini,
kama ni Ndugai atapitishwa, basi ni janga kwani alikuwa Naibu Spika wa
Bunge la 10 ambaye alishindwa kuendana na kasi ya bunge.
Kuhusiana na Dk. Tulia, alisema inasitikisha ,kwani ameshindwa kutimiza
kiapo cha utumishi wa umma na kujiingiza kwenye siasa. Kuhusu Abdullah,
alisema anaamini kuwa umarufu wa baba yake, Rais mstaafu Mwinyi,
umemsaidia kupata nafasi hiyo.
Akizungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanataaluma katika
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA), Nashoni Maisori, alisema kwa maoni
yake, Sitta hakupaswa kupewa nafasi ya kugombea tena uspika kwani
kuongoza kwake Bunge Maalum la Katiba kulitosha kumuondolea sifa.
Mkuu wa Chuo cha Biashara (Aseki), Omary Kiputiputi, alisema kukatwa kwa
Sitta, Nchimbi na vigogo wengine CCM ni jambo la kawaida kwani ndivyo
demokrasia ilivyo na kwamba, wengine walishatumikia serikali kwa muda
mrefu na sasa ni wakati muafaka kwao kupumzika na kulijenga taifa
kupitia maeneo mengine.
Mkazi wa Area C mkoani Dodoma, Gerald Simon, alisema kwa upande wake,
anaamini Sitta ndiye mtu sahihi aliyepaswa kupitishwa na CCM na hivyo
anashangaa kusikia ameenguliwa.
CHANZO:NIPASHE
Post a Comment