Nyota
wa muziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo ‘Jide’MAISHA bwana! Kuna
madai kwamba, nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo
‘Jide’ ambaye ni ‘mtalaka’ wa Mtangazaji Gardner G. Habashi ‘Kapteni’
kwa sasa si kama yule wa zamani akisemekana kuishiwa ‘mpunga’ kiasi cha
mambo yake kwenda halijojo lakini kisa kikuu kikitajwa ni kitendo cha
ndoa yao kuparanganyika.
Kwa
mujibu wa chanzo chetu makini, Jide kwa sasa hana zile mbwembwe zake za
kuonekana mjini akitanua na gari la kifahari kwenye maeneo mbalimbali
ya kujidai kwa vile miradi yake mingi imefunga breki.
MGAHAWA, BENDI VYATAJWA
“Ninachowaambia
ni kweli kabisa jamani! Jide wa sasa si yule wa enzi zile. Nikishibisha
maneno yangu, Jide ameshindwa kuuendeleza Mgahawa wa Nyumbani Lounge
uliopo Kinondoni mpaka ukafulia, hilo mnalijua na kwa sasa mgahawa
unamilikiwa na mfanyabiashara mwingine na ameupa jina lingine.
“Lakini
ukiachana na mgahawa, wewe jiulize, mara ya mwisho kuisikia bendi ya
Jide ya Machozi ikiwa jukwaani ni lini? Pia bendi imesimama! Yaani mambo
yake hayaendi sawasawa kama awali,” kilisema chanzo hicho.
GARDNER KACHANGIA?
Chanzo
hicho kiliendelea kuweka wazi kuwa, baadhi ya marafiki wa zamani wa
familia ya Jide na Gardner wamekuwa wakidai kwamba, kitendo cha wawili
hao kutengana kiliondoa sehemu kubwa ya nguvu iliyokuwa ikisaidia kwenye
biashara.
“Unajua
Gardner licha ya kuwa mumewe, lakini pia alikuwa meneja wake. Ndiye
aliyekuwa akisimamia Bendi ya Machozi na pia alikuwa akisimamia mradi
ule wa mgahawa. Si unajua kwa mambo kama haya, mchango wa Gardner
ulikuwa mkubwa.
“Sasa
kuachana kwao, automatiki Gardner akawa si meneja wa Jide tena, matokeo
yake Jide akashindwa kusimamia miradi yake mwenyewe, ndiyo haya
unayoyaona sasa,” kilisema chanzo.
ATHARI ZA GARDNER ZIMEJIFICHA
Kwa
upande wake, Gardner anatajwa kuendelea na maisha yake vizuri kwani
mpaka sasa ni Mtangazaji wa Kituo cha Redio cha E FM cha jijini Dar
akionekana kutopigika sana na athari za kutengana kwao.
JIDE ALIVYOTAFUTWA
Risasi
Jumatano lilimsaka Jide kwa nguvu zake zote ili kumpa nafasi ya
kufafanua madai hayo lakini kwa simu yake ya mkononi hakuwa hewani.
Risasi
Jumatano lilifunga safari mpaka kwenye makazi anayodaiwa kuishi hivi
sasa maeneo ya Masaki, Dar lakini nyumba hiyo ilionekana kuwa kimya
sana.
Baadhi ya majirani walisema hawajamuona kwa siku kadhaa sasa huku wengine wakisema wanaamini amesafiri nje ya nchi.
“Mh!
Jideee… Jideee! Kwa kweli sijui kama yupo hapa nchini. Inawezekana yupo
lakini pia inawezekana hayupo. Mi binafsi sijamwona siku nyingi,”
alisema jirani mmoja bila kujitambulisha jina.
GARDNER AOMBA UDHURU
Kwa
upande wake, Gardner alipopigiwa simu na kuulizwa kuhusu madai hayo
aliomba udhuru wa dakika kadhaa akisema atapiga yeye ingawa hakufanya
hivyo.
Kumbukumbu
zinaonesha kuwa, mara zote ambazo Gardner amekuwa akipigiwa simu na
waandishi wetu na kuombwa kufafanua kuhusu tuhuma kadhaa, amekuwa
akijibu atapiga yeye baadaye au kusema hana la kuchangia!!
MTABIRI ATIA NENO ZITO
Hata
hivyo, katika moja ya elimu zake za nyota, mtabiri maarufu nchini
ambaye pia ni mtoto wa aliyekuwa mnajimu maarufu Afrika Mashariki,
marehemu Shehe Yahya Hussein, Maalim Hassan alipoulizwa kuhusu maendeleo
ya Jide alisema kuwa, kufifia kwake kunatokana na kutembelea nyota ya
Gardner.
“Yule
alikuwa juu kwa sababu alikuwa akitembelea nyota ya yule aliyekuwa mume
wake. Sasa kwa kuwa waliachana, lazima afifie kwa vile nyota ya yule
ilikuwa kali kuliko yeye,” alisema Maalim Hassan katika mahojiano maalum
nyumbani kwake, jijini Dar es Salaam.
Post a Comment