TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni Mwenyekiti
Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Freeman Mbowe amesema
kuwa hawatashiriki shughuli ya kuapishwa kwa Dk. John Pombe Magufuli
inayotarajiwa kufanyika Alhamis, Novemba 5, 2015.
Kauli
hiyo ya Mwenyekiti Mbowe aliyoitoa leo, imekuja wakati kukiwa bado kuna
sintofahamu kubwa miongoni mwa Watanzania kuhusu mchakato wa uchaguzi
hususan upigaji kura, ukusanyaji na ujumlishaji wa matokeo ulivyofanyika
hasa katika nafasi ya urais.
"Hatutahudhuria
shughuli hiyo ya kumwapisha Magufuli. Tumekubaliana wote kwenye UKAWA,
ndani ya CHADEMA, viongozi wetu, wabunge wetu wote hawatahudhuria
uapishwaji wala sherehe.
"Tumetoa
wito kwa wananchi wote, Watanzania wote, wapenda mabadiliko na wapenda
haki wote kwa ujumla kutohudhuria shughuli hiyo," amesema Mwenyekiti Mbowe.
Mwenyekiti
Mbowe amesisitiza kuwa UKAWA, wapenda mabadiliko wote na Watanzania
wapenda haki hawakubaliani na wanapinga mchakato wa uchaguzi hususan
matokeo ya urais ambayo, kwa mujibu wa Katiba ya Nchi aliyosema ni
mbovu, yakishatangazwa hakuna haki ya kuyapinga katika mahakama yoyote
ile.
"Tunataka
nchi na dunia nzima ijue wazi kuwa hatukubaliani na mchakato wa
uchaguzi hasa matokeo ya urais ambayo kwa mujibu wa Katiba yetu mbovu,
Mwenyekiti wa Tume akishatangaza hakuna mahali pa kuyapinga.
"Matokeo
ya ubunge au udiwani yanaweza kupingwa mahakamani, lakini kwa matokeo
ya urais Katiba yetu mbovu inawafunga mikono na miguu Watanzania wote
ambao wangependa waone haki imetendeka katika nafasi hiyo," amesema Mwenyekiti Mbowe.
'"Watawala
wamechezea haki ya Watanzania kupiga kura. Kura zimehesabiwa kama
karatasi za kawaida tu. Hujuma dhidi ya matokeo ya wagombea wetu
imehujumiwa waziwazi. Safari hii hujuma hazikuwa kificho tena.
"Kila
mtu amejionea matokeo yaliyokuwa na Jaji Lubuva si yale ambaye yalikuwa
yamebandikwa vituoni. Hayakuwa na uhalisia na matokeo yaliyokusanywa na
mawakala.
"Uchaguzi
umefanywa kama ni jambo lisilokuwa na maana yoyote. Hiyo ni hatari sana
kwa taifa lolote linalotaka kukuza demokrasia kama mojawapo ya nguzo za
maendeleo. Hatuwezi kukubali kufika huko," amesema Mbowe.
Aidha,
Mwenyekiti Mbowe ameongeza kusema kuwa vyama vinavyounda UKAWA
vimeitisha kikao cha Wabunge wateule wote wa vyama hivyo ambao
watakutana Alhamis, saa 4 asubuhi, jijini Dar es Salaam.
Imetolewa leo Jumatano Novemba 4, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
Post a Comment