Mjadala
kuhusiana na hatma ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofutwa na Jecha,
umechukua sura mpya, baada ya mmoja wa watoto wa Rais wa zamani, Dk. Amani Abeid Karume, kuibuka na kufichua kile anachoamini kuwa ni sababu ya utata uliojitokeza sasa.
Mtoto huyo ni Mwanasheria, Fatma Karume, ambaye
akiwa pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS), Awadh
Ali Said, waliuambia umma kupitia mahojiano ya moja kwa moja kwenye
kituo kimoja cha televisheni jijini Dar es Salaam juzi kuwa sababu
mojawapo ya kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar ni muundo wa uongozi
unaomruhusu rais wa visiwa hivyo kuwa mmoja wa wajumbe katika Baraza la
Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akifafanua,
Fatma alisema kuwapo kwa nafasi ya moja kwa moja ya Rais wa Zanzibar
kwenye Baraza la Mawaziri kunaibua mgongano inapotokea mshindi wa upande
mmoja akiwa ni wa kutoka chama kingine na hiyo ni sababu mojawapo
wanayoamini kuwa imechangia kufutwa kwa uchaguzi na pia kukwaza ukuaji
wa demokrasia visiwani humo.
Alisema
ni dhahiri hali huwa ngumu kwa baraza la mawaziri linaloundwa na watu
wa itikadi ya chama kimoja kuchanganyika na mwingine mwenye itikadi
tofauti, hasa katika mazingira ya kuwa na usiri katika baadhi ya mambo
na kwamba, hilo huchangia kusuasua kwa maendeleo ya kidemokrasia
visiwani Zanzibar.
Hata
hivyo, ili kuondokana na mgogoro kama uliopo sasa, Fatma alisema ni
muhimu kwa viongozi wa kisiasa nchini na kwingineko barani Afrika
kuzingatia sheria na katiba zilizopo.
Awali,
ilisisitizwa na wanasheria hao kuwa uamuzi wa kufutwa kwa uchaguzi wa
Zanzibar uliochukuliwa na Mwenyekiti wa Zec peke yake, haukuzingatia
sheria na katiba na ndiyo maana sasa kumeibuka mgogoro wa kikatiba kwani
kifungu kinachotumika kuhalalisha hoja ya kuendelea kubaki madarakani
kwa Dk. Shein kimekuwa kikitafsiriwa vibaya kwa maslahi ya kisiasa.
Akielezea
zaidi, Awadh alisema hakuna kifungu chochote kinachomruhusu Jecha
kufuta uchaguzi na ndiyo maana hadi sasa hakuna mtu aliyethubutu kutaja
kwa uwazi ni sheria ipi imempa nguvu mwenyekiti huyo wa Zec kufuta
uchaguzi wa Zanzibar.
Chanzo:mwananchi
Post a Comment