Ushiriki
wa aliyekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Tulia Ackson katika
masuala ya siasa na hatimaye kuchaguliwa Naibu Spika wa Bunge, umezidi
kuibua maswali huku akidaiwa kuwa amekiuka kanuni za watumishi wa umma.
Wasomi,
wanaharakati na wanasheria wameeleza kushangazwa na uteuzi huo, kama
ilivyokuwa Alhamisi alibobanwa kwa maswali bila majibu kuhusu ni lini
msomi huyo wa sheria alichukua kadi ya CCM na kuwania uspika na baadaye
unaibu spika kupitia chama hicho.
Hata
hivyo, Dk Ackson amekanusha kukiuka kanuni za utumishi wa umma akisema
ile inayolalamikiwa kukiukwa (Kanuni za Utumishi wa Umma 2009), ilifutwa
kupitia waraka mpya uliotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Januari, mwaka
huu.
“Angalia
hiyo ‘circular’ kifungu cha (5), kinasemaje, usiangalie hiyo kanuni
tena kwani imefutwa na huo waraka, ukisoma unaonyesha wazi. Zote hizo
unazoniambia nilizifahamu kabla ya kuchukua hatua yoyote, sijakurupuka
tu,” alisema.
Wiki
iliyopita Dk Ackson akiwa mwanasheria wa Serikali alichukua fomu ya
kuwania uspika wa Bunge kinyume na matakwa ya kanuni za utumishi wa
umma, lakini baadaye alijitoa katika kinyang’anyiro hicho na kuwania
unaibu spika, baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge.
Mchakato
wa Dk Ackson kuteuliwa kugombea hadi kushika nafasi hiyo umezua maswali
watu mbalimbali wakihoji ukiukaji wa kanuni hiyo inayozuia wanasheria
wa Serikali kujiunga na mambo ya siasa.
Akijibu
maswali ya wabunge wakati akiomba kuchaguliwa kuwa naibu spika, Dk
Ackson alishindwa kueleza ni lini alichukua kadi ya CCM, hadi Spika wa
Bunge Job Ndugai alipoingilia kati akamruhusu kwenda kuketi.
Wachambuzi
Akizungumzia
suala hilo, mwanaharakati kutoka HakiElimu, Godfrey Bonaventure alisema
kitendo cha Dk Ackson kuteuliwa kushika nafasi hiyo kinaleta maswali
mengi katika kanuni za utumishi wa umma na masuala ya siasa.
“Miongozo
iliyopo imeweka bayana kuwa wapo watumishi wa umma ambao hawatakiwi
kujihusisha na siasa kutokana na unyeti wa majukumu yao,” alisema.
Alisema suala kubwa ambalo Dk Ackson anatakiwa kujibu kwa usahihi ni je, lini alianza kuwa mwanachama wa CCM?
“Watu
wanaotakiwa kuhusika kwenye uamuzi mkubwa hawatakiwi kujihusisha kwenye
siasa. Hili suala lina mitego ambayo inavuruga mfumo wetu wa
uwajibikaji, inatupa shaka kwa sababu hawa watu maamuzi yao ni magumu,
uspika ni wajibu mkubwa,” alisema.
Bonaventure aliitaka Serikali kuheshimu miongozo yote ya utumishi wa umma ili vyombo hivyo viwe huru kufanya uamuzi.
“Alipoulizwa
swali bungeni kuhusu lini alikuwa mwanachama wa CCM hakuweza kutoa
jibu sahihi, bila shaka angesema ni lini angeibua maswali mengi zaidi,”
alisema.
Alisema
iwapo Dk Ackson angesema amekuwa mwana CCM kwa muda mrefu angeibua
maswali, lakini pia angesema amechukua kadi ya CCM hivi karibuni
angeibua hoja atawezaje kukifahamu chama na kujua namna ya kuliongoza
Bunge katika kipindi kifupi?
Mwanasheria
wa kujitegemea, George Shayo alisema sheria inaweka wazi kuwa watumishi
wa Serikali hawatakiwi kushiriki katika siasa.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema sheria zinakataza watumishi wa umma kujihusisha na siasa.
Profesa
Safari ambaye pia ni wakili, alisema ingawa baadhi ya vipengele
vimefanyiwa marekebisho lakini wafanyakazi wa Mahakama na wanasheria wa
Serikali hawatakiwi kujihusisha na siasa.
“Ndiyo
maana hata wakati Jaji Augustino Ramadhani alipochukua fomu ya urais,
tulimsema sana. Hata hizi sarakasi za Dk Ackson zinachekesha,
zinashangaza,” alisema.
Mhadhiri
wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander
Makulilo alisema anafahamu kuwa kuna sheria kuhusu wafanyakazi wa umma
lakini haiwakatazi kujihusisha na siasa bali upo utaratibu wa kufanya
hivyo.
“Iko
miongozo ya Serikali kuhusu watumishi wa umma lakini si kwamba sheria
inakataza, kwa mfano miongozo hiyo inawataka waache nafasi zao pindi
wanapotaka kuingia katika siasa,” alisema.
Post a Comment