Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini Bi.
Badra Masoud akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani)mapema leo jijini
Dar es Salaam kuhusu mpango wa Serikali wa kuunda kikosi maalum cha kukabiliana
na tatizo la wizi wa umeme na kuimarisha ukaguzi ili kubaini wateja wasio
waaminifu na kuwachukulia hatua za kisheria. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara
ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa. (Picha na Fatma Salum- Maelezo).
Serikali yajipanga kukabiliana na Wizi wa
Umeme Nchini.
Na. Fatma Salum - MAELEZO
Serikali inatarajia kuunda kikosi maalum
kitakachojumuisha wataalam kutoka taasisi mbalimbali ili kukabiliana na tatizo
la wizi wa umeme linalopelekea Shirika la Umeme (TANESCO) kukosa mapato
inavyostahili.
Hayo yamebainishwa na Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini Bi.
Badra Masoud wakati akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari leo
jijini Dar es Salaam.
Bi. Badra amesema kuwa kutokana na wizi wa
umeme kukithiri na kuliingizia hasara Shirika la Umeme (TANESCO), Wizara itaunda kikosi hicho kitakachojumuisha
wataalam kutoka TANESCO, Wizara ya Nishati na Madini na Vyombo vya Usalama ili
kukabiliana na tatizo hilo.
“Aidha Wizara ya Nishati na Madini
imeliagiza shirika la TANESCO kuimarisha kikosi chake cha ukaguzi wa watumiaji
wa umeme ili kubaini wateja wasio waaminifu wanaoiba umeme na kuwachukulia
hatua za kisheria.” Alisema Badra.
Kwa upande mwingine Serikali imezitaka
Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali kuzingatia matumizi bora
ya umeme ili kudhibiti upotevu wa nishati hiyo muhimu kwani imebainika kuwa
kuna baadhi ya ofisi wana kawaida ya kuacha wazi vifaa vya umeme baada ya muda
wa kazi vikiwemo vifaa kama kompyuta, AC na taa.
Aidha Bi. Badra ameongeza kuwa Serikali
inatoa onyo kwa watu wanaohujumu miundombinu ya TANESCO ikiwemo kuchoma nguzo
za umeme na kuiba mafuta ya transfoma kuacha mara moja kwani wakigundulika
hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Akizungumzia hali ya umeme nchini Bi. Badra
amesema kuwa hali ni nzuri na hakuna mgawo wowote kwa sasa kwani kasi ya
uzalishaji wa umeme ni nzuri na kiasi kinachopatikana sasa ni megawati 1500
huku matumizi yakiwa ni kati ya megawati 800 na 900 kwa siku.
Post a Comment