Ndugu zangu,
Historia ni Mwalimu Mzuri. Nimelisema hilo mara kadhaa.
Wakati
fulani mwaka 1984, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar walikutana
pale Kisiwandui chini ya Alhaj Aboud Jumbe, aliyekuwa Rais wa Zanzibar
na Makamu wa Rais wa JMT.
Ndani ya
kikao kile walikuwamo wanasiasa wa aina ya Ramadhan Haji Fakhi, huyu
alikuwa Waziri Kiongozi, alikuwamo pia Hamad Rashid, Hamis Shabaan Mloo,
na Seif Sharif Hamad.
Wajumbe
walizungumza jasho likiwatoka juu ya hali isiyo sawa kwenye Muungano
yakiwemo madai kuwa Zanzibar haikuwa hata na fursa ya kukopa nje ya nchi
kwa vile imo ndani ya Muungano.
Ikajengwa hoja ya Serikali Tatu. Wajumbe wote wakaafiki. Ikafika siku ya kuwasilisha hoja Dodoma.
Ajabu ya jambo lile, Julius Nyerere, alionekana kulijua hilo mapema sana. Alhaj Jumbe mkutanoni Dodoma akawa na wakati mgumu.
Wenzake wote akiwamo Seif Sharif Hamad waliikana hoja isipokuwa Ramadhan Haji Fakhi, Waziri Kiongozi.
Inasemwa, Julius Nyerere alimuuliza Ramadhan Haji Fakhi;
" Moja jumlisha moja ni ngapi?"
Jibu: " Tatu!"
" Moja jumlisha moja ni ngapi?"
Jibu: " Tatu!"
Inasemwa
pia, Julius Nyerere aliwachekesha wajumbe alipohoji ni shule gani
aliyesoma Ramadhan Haji Fakhi yenye kufundisha hesabu kwa namna hiyo!
Hatma ya
kikao kile cha Dodoma ni Alhaj Jumbe kuvuliwa nyadhifa zake zote ndani
ya chama ikiwamo kuachia Urais wa zanzibar. Ramadhan Haji Fakhi pia
akunusurika, alikwenda na maji.
Ali Hassan Mwinyi akafanywa kuwa Rais wa Zanzibar na Seif Sharif Hamad akawa Waziri Kiongozi.
Mwaka
mmoja na nusu baadae, mwaka 1985, Ali Hassan Mwinyi akateuliwa kuwa
mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano na akawa Rais kwa kuchaguliwa na
Wananchi.
Inasemwa, kwa vile Ali Hassan Mwinyi alipata fursa hiyo, basi, Seif Sharif Hamad alitumaini angekuwa Rais wa Zanzibar.
Hapana,
CCM ikamteua Idrissa Abdul Wakil kugombea nafasi ya Rais wa Zanzibar.
Seif Sharif Hamad akawa ameukosa Urais na akafanywa kuwa Waziri
Kiongozi. Kukawa na minong'ono ya Seif kulalamika chini chini.
Ikafika
wakati kukawa na ' Hali ya Hewa ya kisiasa Iliyochafuka Visiwani'.
Nilikuwa mwanafunzi pale Tambaza Sekondari. Ilinong'onwa mjini kuwa Rais
wa Zanzibar, Abdul Wakil, kutokana na hali ya hewa kuchafuka, akawa
anafanya kazi Unguja na anarudi kulala Dar es Salaam.
Siku moja
wakati nikitoka shule na kupita maeneo ya Upanga kuelekea kituo cha
mabasi cha Palm Beach, kwenye moja ya nyumba za eneo hilo, nikamwona kwa
macho yangu Rais wa Zanzibar, Idrissa Abdul Wakil. Nikafahamu baadae,
kuwa aliishi kwenye moja ya nyumba za eneo hilo.
Mwaka
1988, akina Seif Sharif Hamad , Hamad Rashid na wenzao, walitaka hoja ya
Serikali Tatu ipelekwe tena Dodoma. Safari hii Idrissa Abdul Wakil
aliipinga kutokana na uzoefu wa 1984.
Seif
Sharif Hamad naye akaishia kupokonywa kadi yake ya uanachama CCM.
Vuguvugu la mageuzi ya kisiasa duniani likaanza kwenye kipindi hicho.
Lilitokea Ulaya Mashariki.
Ndipo
akina Seif Sharif Hamad wakapata fursa ya kuanzisha KAMAHURU. Na baadae
CUF ikaja pia. Na ndoto ya Seif Sharif Hamad ikabaki hai, ndoto ya siku
moja kuwa Rais wa Visiwa vya Zanzibar.
Mwaka huu
wa 2015, Seif Sharif Hamad amerusha tena karata yake. Anaweka rekodi,
ya kuwa mgombea mkongwe kushinda wote, na mwenye uzoefu wa kugombea
Urais kwa zaidi ya miaka 20. Kuna tunachojifunza.
Ndugu zangu Wajumbe,
Nimejaribu kukumbuka hayo. Nakaribisha maoni yenu pia...
Maggid.
Post a Comment