Chama
cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar
hauwezi kupatikana kwa kutumia nguvu au vitisho vya kuingiza vifaru na
magari ya maji ya kuwasha, kama inavyotokea sasa; bali kinachotakiwa ni
meza ya majadiliano.
Tamko hilo limetolewa na mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Aliwataka
wafuasi wa CUF na wananchi kuendelea kuwa na subira wakati viongozi wao
wakiwa katika jitihada za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
Alisema
mgogoro uliojitokeza Zanzibar ni mgogoro wa kisiasa baada ya haki ya
kidemokrasia ya wananchi kupindishwa ndio maana CUF inataka Mwenyekiti
afute uamuzi wake, amalizie kazi iliyobakia ya kuhakiki matokeo na
kutangaza mshindi.
"Tatizo
lililopo ni la kisiasa na ufumbuzi wake si vifaru wala kuongeza ulinzi,
linahitaji njia ya mazungumzo kumalizika kwake," alisema.
Aidha,
Maalim Seif aliwataka wanachama kuendelea na utulivu kutokana na juhudi
zinazofanywa na Jumuiya za Kimataifa kuonesha mwelekeo wa kupatikana
ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar.
Alisema
CUF inaimani kwamba ufumbuzi wa haki wa suala hilo hauko mbali na
Wazanzibari wataona mafanikio ya demokrasia yatakayojengwa nchini.
Alisema haki lazima itendeke katika uchaguzi uliopita.
"Sisi
tumepata moyo na imani kwamba ufumbuzi wa haki wa suala hili hauko
mbali na Wazanzibari wataona mafanikio ya demokrasia yetu tunayoijenga
katika nchi yetu," alisisitiza Maalim Seif.
Aliwaomba
Wazanzibari wote wanaopenda amani wawe waangalifu sana na taarifa za
uongo zinazotolewa za kuchochea kufanya vurugu kwa kisingizio kuwa
zimetolewa na viongozi wa CUF wakati ni uongo.
"Nitumie
fursa hii kuwashukuru wale wote wanaofanya juhudi kubwa kuona ufumbuzi
wa haki na wa amani unapatikana kwa tatizo hili lililosababishwa na mtu
mmoja aliyeamua kuacha wajibu wake na kutumikia maagizo ya kikundi cha
watu wabinafsi", alisema.
Aidha,
alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar,
Dkt. Ali Mohamed Shein, bado wana nafasi kubwa ya kuhakikisha
wanaivusha Zanzibar kwa kumaliza mgogoro wa uchaguzi uliojitokeza kwa
amani na utulivu.
"Kwa
mara nyingine tena natoa wito kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais Dkt Shein
kuchukua dhamana ya uongozi na kwa pamoja tushirikiane kuikwamua
Zanzibar na Tanzania katika mkwamo huu", alisema.
Alisema
kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vina wajibu mkubwa wa kusaidia
kupatikana ufumbuzi wa tatizo walilonalo badala ya kuongeza wasiwasi kwa
wananchi wao waliotulia.
Akizungumzia
kuhusu uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim
Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar, alisema kuwa wamepata
taarifa kuwa Mwenyekiti huyo ameitisha kikao cha Tume na kuwataka
makamishna kuunga mkono uamuzi wake huo alioutangaza pekee wa kufuta
matokeo ya uchaguzi.
Alisema
kuwa ni vyema kwa Mwenyekiti huyo akatambua kwamba hata akiwatumia
baadhi ya makamishna kumuunga mkono, bado uamuzi huo hautakuwa halali
kwa sababu haumo katika uwezo uliopewa Tume; si katiba wala sheria ya
uchaguzi.
"Kwa
ufupi suala hili halina njia nyingine ya kulimaliza zaidi ya
kukamilisha kazi ya kufanya majumuisho, kuhakiki matokeo na kumtangaza
mshindi wa uchaguzi", alisema Maalim Seif.
Maalim
Seif aliwahakikishia viongozi na wanachama wa CCM kwamba hawana sababu
ya kuwa na hofu na maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya Oktoba 25 mwaka
huu; na kwamba kama kuna tofauti zozote za kisera na kimtazamo baina yao
zinaweza kuzungumzwa na maelewano kufikiwa.
"Nawahakikishia
viongozi na wanachama wa CCM na Wazanzibari wote kwamba hakutakuwa na
ulipizaji kisasi au kufukua makaburi kwa mambo yaliyopita, sote
tutafanya kazi pamoja bila ya kujali tofauti za itikadi za kisiasa,
asili, kabila au dini zetu, Zanzibar ni moja na itabaki kuwa moja," alisisitiza Maalim Seif.
Post a Comment