Kushindwa kwa mgombea wa
urais wa Chadema kupitia Ukawa, Edward Lowassa kumesababisha vijana
wengi katika Jimbo la Lulindi mkoani Mtwara kususia uchaguzi mdogo wa
mbunge jana.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya vijana wa
jimbo hilo, Jafari Hamisi, Nurudini Majaliwa na Saidi Mohamed walisema
sababu kubwa ya kususia kuchagua mbunge ni kutoridhishwa na mfumo wa
siasa ambao walidai hauzingatii demokrasia ya vyama vingi, bali
umeegemea chama kimoja pekee.
Mkazi wa Kata ya Lulindi, Anasa
Hussein alisema watu wengi wamekatishwa tamaa kutokana na kuahirishwa
kwa uchaguzi huo Oktoba 25.
“Mimi kwa upande wangu sikujua leo
kama unafanyika uchaguzi wa mbunge, nilikuwa najiandaa kwenda shambani,
nikasikia watu wanasema leo ni siku ya uchaguzi, " alisema Anasa.
Msimamizi
wa uchaguzi wa Jimbo hilo, Beatrice Dominic amekiri kuwapo mwitikio
mdogo wa wapiga kura licha ya kufanya uhamasishaji mkubwa.
Msimamizi
wa Kituo cha Zahanati ya Chiungutwa, Romanusi Charles alisema mwamko wa
kupiga kura ulikuwa mkubwa kwa vijana katika uchaguzi wa Oktoba 25
kwani wengi walijitokeza tofauti na jana.
Mgombea ubunge wa NLD,
Modester Makaidi alisema katika vituo ambavyo alitembelea, vijana
walishindwa kujitokeza kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura.
Mgombea wa CCM, Jerome Bwanausi jana asubuhi aliendelea kusisitiza wananchi kujitokeza kupiga kura katika vituo vyao.
Post a Comment