Umoja wa Mataifa umethibitisha kwamba walinda amani 14 wa muungano huo waliuawa na wengine 53 kujeruhiwa baada ya kambi yao kuvamiwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kati ya waliouawa, angalau wanajeshi 12 walitoka Tanzania.
Katibu mkuu huyo ameshutumu vikali shambulio hilo na kusema ni sawa na uhalifu wa kivita.
Ameitaka DR Congo kufanya uchunguzi kuhusu shambulio hilo na kusema kwamba waliohusika wanafaa kuwajibishwa.
Wanajeshi zaidi wametumwa eneo hilo na kamanda wa kikosi cha kulinda amani anaelekeza shughuli ya kuwaondoa majeruhi.
Bw Guterres amesema shambulio hilo ndilo mbaya zaidi kuwahi kutekelezwa dhidi ya walinda amani wa UN katika historia yake miaka ya karibuni.
"Ningependa kueleza kusikitishwa kwangu na shambulio hilo lililotekelezwa usiku wa jana dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini DRC."
"Taarifa za mwanzo mwanzo eneo la shambulio eneo la Kivu Kaskazini zinaonesha angalau walinda amani 12 kutoka Tanzania waliuawa na wengine 40 kujeruhiwa, wanne vibaya.
"Na tunafahamu pia kwamba wanajeshi watano wa jeshi la DR Congo waliuawa.
"Natuma salamu zangu za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa waathiriwa na pia kwa serikali na watu wa Tanzania.
Na nawatakia uponaji wa haraka wote waliojeruhiwa."
Shambulio hilo lilitekelezwa Alhamisi jioni kwenye kambi ya jeshi ya Semuliki eneo la Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema wanajeshi 5 wa jeshi la DR Congo (FARDC) waliuawa pia kwenye shambulio hilo.
Umoja wa Mataifa unasema waasi wa ADF ndio wanaotuhumiwa kutekeleza shambulio hilo.
"Natuma salamu zangu za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa wanajeshi wa kulinda Amani na wanajeshi wa FARDCwaliouawa au kujeruhiwa," amesema mwakilishi mkuu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DR Congo ambaye ndiye pia mkuu wa kikosi cha walinda amani ambacho hufahamika sana kama Monusco.
Awali, katibu mkuu msaidizi wa Umoja wa Mataifa anayeangazia masuala ya kulinda amani alikuwa ameandika kwenye Twitter kwamba "idadi kubwa" ya wanajeshi walikuwa wameuawa.
Bw Jean-Pierre Lacroix alisema wanajeshi zaidi wametumwa eneo hilo na majeruhi wanasafirishwa.
Waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) chimbuko lao ni Uganda lakini wametuhumiwa kutekeleza mashambulio na visa vya ukatili eneo hilo la DR Congo.
Post a Comment